Mkurugenzi wa bendi ya African Stars, 'Twanga Pepeta' Asha Baraka, (kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utambulisho wa onyesho maalum la mwamamuziki mkongwe, Muhidin Gurumo (53) wa pili kutoka kwa Asha. Onyesho hilo maalum litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, limetambulishwa leo jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Gurumo ni Juma Mbizo na Said Kibiriti.
Mkutano huo ukiendelea.....
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo leo.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI mkongwe ambaye hivi karibuni alitangaza rasmi kustaafu kufanya shughuli za kimuziki na kuimba akiwa na bendi ya Msondo Ngoma, Muhdini Gurumo, ameandaliwa maonyesho mawili maalum kwa ajili ya kumuaga rasmi katika tasnia hiyo ya kimuziki.
Kati ya maonyesho hayo moja limepangwa kufanyika Oktoba 11, ikiwa kwa ajili ya VIP, litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Na onyesho jingine litafanyika Novemba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, ambapo maonyesho yote yakiwa na lengo la kumuaga kwa heshima baada ya mwanamuziki huyo kutangaza kuachana na muziki rasmi na kumpa nafasi ya kumudu maisha yake baada ya kuachana na muziki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Mwenyekiti wa Onyesho hiloiliyopewa jina la (Gurumo 53), Asha Baraka, alisema kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa maonyesho hayo maalum ya kumchangia fedha mkali huyo.
Aidha alisema kuwa, wazo hilo limefanyiwa kazi kwa pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard Sakala mjumbe, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo, ambaye ndio mratibu wa Kamati hiyo.
"Lengo si kumpa karatasi za kuthamini mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, bali ni kuhakikisha kuwa anapata mwangaza wa maisha yake baada ya kuachana na muziki.
"Huyu ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu wa kufanya kazi hadi alipotangaza kustaafu, hivyo kwa sasa ni lazima sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika ramani nzuri, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuusongesha muziki wa Tanzania,” alisema. Naye Gurumo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameamua kuachana na muziki kwasababu umri na afya yake hairuhusu kufanya kazi hiyo, hivyo asitokee mtu wa kupotosha ukweli wake huo.
"Nasikia watu wanasema naachana na muziki Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena Sikinde, jambo ambalo si kweli kwakuwa sioni nitamuimbia nani wakati nimechoka".alisema
”Naomba kwa sasa kuwapa nafasi watu waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda kamati hii ambayo nitapanda jukwaani kuimba mara ya mwisho, ukizingatia kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na mashabiki wangu jukwaani na si mahali pengine,” alisema.
Katika hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas Chidumule, alisema kuwa licha ya kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na mzee Gurumo kama sehemu ya kutambua mchango wake na kukumbukia enzi zao.
”Nimeokoka lakini si sababu ya kunifanya nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye nina uhakika mchango wake ulinifanya niwe juu katika muziki wa dansi Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo ambayo Mdoe ndio Katibu wake, taratibu zote zinaendelea ikiwa ni kuandaa nyimbo alizowahi kuimba na kuziweka katika mfumo wa kibiashara, ikiwamo mpango wa kuuda nyimbo zake katika makampuni ya simu za mikononi.
No comments:
Post a Comment