Wednesday, May 16, 2012
MILLIONI 900 KUDHAMINI CECAFA 2012
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki (Cecafa) limesema mashindano ya Kombe la Kagame mwaka huu yatakayofanyika jijini Dar es Salaam, yatagharimu dola 600,000 (sawa na Sh944 milioni).
Mwaka jana mashindano hayo yalidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania TBL kupitia bia yake ya Castle kwa Sh300 milioni.
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alisema hayo wakati akifafanua bajeti ya mwaka huu ya mashindano hayo.
Akijibu maswali aliyoulizwa na gazeti la East African Business Week, Musonye alisema kwa asilimia kubwa, maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika."Hivi sasa tunasubiri timu kuthibitisha ushiriki wao ili tuweze kupanga ratiba ya timu 12 zizotarajia kushiriki mwaka huu," alisema Musonye.
Musonye aliwataka mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo yatakayofanyika Tanzania kwa mara ya tatu mfululizo, ambapo pia yataonyeshwa katika kituo cha televisheni cha Super Sport.
Mashindano hayo yamekuwa yakidhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame tangu mwaka 2002. Kabla ya udhamini wa Kagame, mashindano yakijulikana kama Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na yalianzishwa mwaka 1974.
Musonye alisema mashindano hayo yanafanyika tena Tanzania kwa sababu ya mafanikio yaliyopatikana katika mashindano ya Kombe la Chalenji na Kombe la Kagame mwaka jana.Pia uhakikia wa udhamini ndiyo uliopelekea mashindano hayo kufanyika tena Dar es Salaam, alisema zaidi Musonye.
Mwaka jana mashindano hayo yalitakiwa kufanyika Zanzibar, lakini kwa sababu ya ukata yakahamishiwa Sudan ambayo nayo ilishindwa kuwa mwenyeji wka sababu ya matatizo ya kisiasa.
Hivyo Cecafa iliamua mashindano hayo yafanyike jijini Dar es Salaam, ambapo yalikuwa na mafanikio kwa sababu mapato ya viingilio yaliyopatikana kwenye mechi za mashindano hayo yalikuwa sh 1.2 bilioni (dola 763,358).
Mashindano hayo ya Kagame yalikuwa na mvuto zaidi kuanzia hatua za robo fainali katika mechi tofauti zilizocheza timu za Simba na Yanga.
Mashabiki wa soka wa Afrika Mashariki walijikuta wakiacha kuangalia mechi za Ligi Kuu ya England na kufuatilia mechi za mashindano ya Kombe la Kagame mwaka jana hasa hasa kuanzia hatua ya robo.
Mwaka jana timu 13 zilishiriki, ambazo ni Ulinzi (Kenya), Ports (Djibouti), St George (Ethiopia), El Merreikh (Sudan), Red Sea (Eritrea), Elman (Somalia), APR na Etincelles (Rwanda), Bunamwaya (Uganda), Vital'O (Burundi) na wenyeji Simba na Yanga za Tanzania.
Mabingwa watetezi wa michunao hiyo ni Yanga iliyoifunga Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali, shukrani kwa bao pekee la dakika za majeruhi kutoka kwa mshambuliaji Ghana, Kenneth Asamoah.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment