Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento akionyesha ripoti ya Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam..
Msajili wa Vyama vya siasa, John Tendwa.
Michael Kamuhanda, RPC wa Iringa
Mwangosi akishambuliwa na rundo la Polisi kabla ya kuuawa kwa bomu.
Polisi wakionekana pembeni ya mabaki ya mwili wa marehemu Mwangosi
Mabaki ya mwili wa Mwangosi yakionekana huku aliyeketi akiwa ni polisi aliyejeruhiwa pia na bomu lililomuua.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kamati ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Kajubi Mukajanga wa MCT (kulia) akionyesha ripoti ya mauaji ya Mwangosi juzi. Kushoto ni Mhariri wa gazeti la NIPASHE aliyekuwa akiwakilisha Jukwaa la Wahariri, Jesse Kwayu. |
Vilevile, Tume hiyo
inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Kiongozi mstaafu, Amiri Manento, pia
imebaini kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alikiuka misingi ya
utawala bora kwa kutoa maelekezo yanayokinzana na Sheria ya Takwimu namba 1 ya
mwaka 2002.
Ripoti ya Tume hiyo iliwekwa
hadharani na Jaji Manento, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Jaji Manento alizitaja haki
za binadamu zilizovunjwa na jeshi hilo
wakati wa operesheni yake hiyo kuwa ni pamoja na haki ya kuishi; haki ya
kutoteswa na kutopigwa; haki ya usawa mbele ya sheria; na haki ya kukusanyika
na kutoa maoni.
Alisema haki hizo za binadamu
zinalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu, Mkataba
wa Kimataifa kuhusu Haki ya Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Mataifa ya Afrika
kuhusu Haki za Binadamu na Watu.
Alisema ili kuwako utawala
bora mamlaka zote za serikali ni lazima zifuate utawala wa sheria.
Hata hivyo, alisema uchunguzi
umebaini kuwa Kamanda Kamuhanda Septemba 2, mwaka huu, katika utekelezaji wa
majukumu yake, alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu
cha 11 (a) na (b) na Sheria ya Polisi (Sura 322).
Jaji Manento alisema Kamanda
Kamuhanda alikiuka sheria hizo kwa kuingilia kazi za Mkuu wa Polisi Wilaya
(OCD) ya Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za Chama cha Demoklrasia na
Maendeleo (Chadema) wakati yeye (Kamuhanda) hakuwa kiongozi wa polisi wa eneo
husika.
“Kwa maana hiyo amri
aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka
kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” alisema Jaji Manento.
Kwa mujibu wa Jaji Manento,
wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Chadema katika Kata ya Nyololo, Wilaya
ya Mufindi ukiendelea, Kamanda Kamuhanda alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa Chadema
wakamatwe, hali iliyowafanya wafuasi wa chama hicho kupinga kukamatwa kwa
viongozi wao.
Jaji Manento alisema mbali na
kutoa amri hiyo, Kamanda huyo aliamuru pia kupigwa kwa mabomu ya machozi ili
kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi la Chadema.
Aidha, alisema hatua ya
Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha
shughuli zao kwa sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora, kwani
maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hizo yalikinzana na Sheria ya Takwimu
namba 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati
wa sensa.
Alisema hatua hiyo ya Tendwa
pia ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11
(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya
kuingiliwa.
Jaji Manento pia alisema
Ibara ya 8 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inaelezea kwamba, Tanzania
ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii.
Alisema pia ibara ya 18 (b)
na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano
(kutoa maoni/habari) na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.
“Haki hii imekiukwa kwa kiasi
kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo, Mufindi kwa kuwa waandishi
wa habari na wafuasi wa Chadema walizuiwa na polisi kufanya shughuli zao za
kupata habari na za kisiasa,” alisema Jaji Manento na kuongeza:
“Huu ni ukiukwaji wa misingi
ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha uhuru wa habari.”
Alisema baada ya mabomu ya
machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo na kwamba, marehemu
Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu na
kufa papo hapo.
Jaji Manento alisema Mwangosi
aliuawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo ofisi ya Chadema tawi la
Nyololo.
Alisema katika tukio hilo, wananchi kadhaa
walijeruhiwa kwa mabomu, akiwamo mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE,
Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chadema Wilaya ya Mufindi,
Winnie Sanga, na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi, Asseli Mwampamba, aliyekuwa
akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Mwangosi.
“Kutokana na hayo yote, Tume
imejiridhisha kuwa tukio lililosababisha kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na
uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” alisema
Jaji Manento.
Alisema Chadema ni chama cha
siasa, ambacho kina usajili wa kudumu na kwamba, chini ya Sheria ya Vyama vya
Siasa, vyama vyenye usajili wa kudumu vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa
na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa ofisa wa polisi wa eneo
husika.
Jaji Manento alisema baada ya
taarifa kutolewa, chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi.
MAONI NA MAPENDEKEZO
Aliitaka Kamati za Ulinzi na
Usalama za Mkoa na Wilaya kuwa makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za
binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora vinavyofanywa na mamlaka
mbalimbali kwenye maeneo yao.
Pia kamati hizo zihusike moja
kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote
ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
Pia aliwatakwa viongozi wa
Chadema na wafuasi wao kuepuka malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo
yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti.
Alisema pale wanapogundua
kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara
makubwa yanayoweza kutokea.
Pia alilitaka Jeshi la Polisi
na Msajili wa Vyama vya Siasa kuepuka kufanya maamuzi au matendo yanayoibua
hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu
yao ya
kisheria.
“Mfano, Jeshi la Polisi
lilizuia mikutano ya Chadema kwa sababu ya sensa wakati huo huo Chama Cha
Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar,” alisema Jaji Manento na kuongeza:
“Rai ya Msajili wa Vyama vya
Siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku Chadema walishurutishwa na
Polisi kutii rai hiyo."
Pia alitaka demokrasia ya
vyama vingi iheshimiwe na kulindwa na elimu ya vyama vya siasa na sheria ya
polisi kuhusu vyama hivyo itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana
kutozifahamu kabisa.
WANAHARAKATI WAPONDA RIPOTI
Wanaharakati wameponda ripoti
ya Kamati ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi iliyowasilishwa juzi na mwenyekiti
wake, Jaji Stephen Ihema, na kusema kuwa yanatia aibu kwa jamii.
Mkurugenzi wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alitoa maoni hayo
jana katika maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani yaliyofanyika
jijini Dar es Salaam.
Alisema matokeo
yaliyotangazwa juzi na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk.
Emanuel Nchimbi kuchunguza chanzo cha kifo hicho ni ya hovyo kwa kuwa
yameonyesha namna ambavyo polisi wanavyolindana.
Alisema jamii yote inajua
namna polisi ilivyohusika kumuua Mwangosi, lakini anashangaa kusikia matokeo ya
uchunguzi yakiwaweka kando.
Ingawa alisema hajasoma
ripoti kamili ya kamati hiyo, lakini alisema kwa matokeo hayo yanatia wasiwasi
na kwamba picha zilizoonyesha tukio lile zilitoka wapi.
Alisema kesho kituo chake
kinatarajia kutoa msimamo kamili juu ya tukio hilo la kinyama ambalo lilifanywa na polisi.
Ripoti ya jana ya Tume ya
Utawala Bora ni ya tatu kuwekwa hadharani. Ya kwanza ilikuwa ya Baraza la
Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri (TEF) ambayo iliwaona polisi kuwa
wahusika wakuu wa mauaji hayo huku RPC Kamuhanda akielezwa kuwa alisimamia
mauaji hayo moja kwa moja.
Ripoti ya MCT na TEF
ilitolewa siku moja na ya Kamati ya Waziri Nchimbi, zikikubalina kuwa kulikuwa
na uhusiano mbaya baina ya waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa na polisi,
lakini ile ya kwanza (MCT na TEF) ikithibitisha kuhusika kwa polisi katika
mauaji wakati ya Waziri Nchimbi ikikwepa ukweli huo. Soma Muhtasari wa Ripoti
ya Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu uk. 14.
No comments:
Post a Comment