MGANGA mmoja wa kienyeji nchini Ghana amedai kuwa yeye ndio aliyemsababishia matatizo ya majeruhi Cristiano Ronaldo ambayo hayataweza kutibika kwa daktari yoyote. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid anasumbuliwa na majeraha ya goti na kuna uwezekano akakosa mechi za kirafiki kwa ajili ya kujipima nguvu ambazo Ureno itacheza na Mexico na Ireland. Mganga huyo aitwaye Nana Kwaku Bonsam amedai majeraha aliyonayo Ronaldo ni kimazingara zaidi hivyo hawezi kutibika hospitali. Akihojiwa Bonsam amesema anajua kuhusu majeruhi ya Ronaldo kwasababu yeye ndio anafanyia kazi suala hilo na kuongeza kuwa wiki iliyopita alienda kutafuta mbwa wanne kwa ajili ya kutengeneza dawa maalumu iitwayo “Kahwiri Kapam”. Mganga huyo aliendelea kudai miezi minne iliyopita alisema kwamba atamtengeneza nyota huyo ili asicheze michuano ya Kombe la Dunia au kumzuia asicheze mechi dhidi ya Ghana na jambo kubwa analoweza kufanya kumuweka nje ni kuhakikisha anakuwa majeruhi. Ghana inatarajiwa kucheza na Ureno Juni 26 jijini Brasilia mchezo ambao utakuwa wa mwisho katika kundi lao la G ambalo pia lina timu za Ujerumani na Marekani.
No comments:
Post a Comment