Chama cha soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimezipongeza timu za taifa za soka, Kilimanjaro Queens iliyofanikiwa kuunyakua ubingwa wa michuano ya Cecafa ya wanawake iliyofanyika mjini Jinja nchini Uganda.
Timu hiyo iliyoiwakilisha Tanzania Bara na ikiwa chini ya kocha mkuu Sebastian Nkoma na msaidizi wake Edina Lema,ilianza mashindano hayo kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ambapo imeisambaratisha Kenya kwa kuifunga mabao 2-1.
Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kasongo amesema kitendo cha Kilimanjaro Queens kutwaa kikombe hicho kinaonyesha ni kwa kiasi gani walivyo tayari kwa ajili ya mapambano,na endapo nguvu kubwa itatumika katika maandalizi yao wanaweza kulitangaza zaidi taifa lao.
Kasongo amelipongeza pia benchi la ufundi kwa uvumilivu mkubwa waliouonyesha tangu walipokabidhiwa kikosi hicho licha ya kuwa muda na matayarisho yao hayakuwa rafiki kiushindani.
Michuano hiyo iliyoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka huu na baraza la vyama vya soka katika ukanda wa afrika mashariki,imeiweka tanzania katika ramani kupitia medani ya mpira wa miguu barani Afrika.
Mbali na timu hiyo ya wanawake, DRFA imeimwagia sifa Serengeti Boys inayosaka tiketi ya kutinga katika michuano ya kuwania kombe la mataifa ya afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika mwezi Aprili nchini Madagascar.
Kikosi hicho chini ya kocha Bakari Shime, kimebakiza mchezo mmoja wa marudiano dhidi ya Congo Brazzaville kabla ya kutinga katika fainali hizo,ambapo katika mchezo wa kwanza wamefanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-2.
Mwenyekiti Kasongo ameongeza kuwa mafanikio ya vikosi hivyo vya taifa ni ya watanzania wote na kuwaomba wachezaji wasibweteke na hali hiyo na badala yake wazidi kujituma ili kuboresha viwango vyao vya kucheza soka na kulisaidia taifa.
IMETOLEWA NA DRFA.
No comments:
Post a Comment