Baada ya kuwa na utata kuhusu Didier Drogba kuendelea kuichezea Nchi yake Ivory Coast, Mchezaji huyo ambaye anabwaga manyanga rasmi mwishoni mwa Juni Klabu yake ya Chelsea alikowapa Ubingwa wa Ulaya Jumamosi iliyopita, amesisitiza kuwa yu tayari kuichezea Nchi yake kwenye Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2014 huko Brazil ikiwa atachaguliwa kwenye Timu ya Taifa.
Drogba, Miaka 34, anategemewa kuitwa na Kocha wa Ivory Coast, Francois Zahoui, kwa ajili ya Mechi ya Mchujo ya Kundi C, Kanda ya Afrika, kuingia Fainali za Kombe la Dunia 2014, dhidi ya Timu ya Taifa ya Tanzania,Taifa Stars, itakayochezwa huko Abidjan, Ivory Coast hapo Juni 2.
Tanzania na Ivory Coast zipo Kundi C pamoja na Morocco na Gambia.
Akiongelea kuhusu kuitumika Nchi yake, Drogba alisema: ‘Sijafikia mwisho wa kuichezea Ivory Coast. Nitacheza Fainali zangu za 3 za Kombe la Dunia huko Brazil Mwaka 2014. Nikiitwa, nitaitika!’
Mbali ya Drogba kuondoa kiwingu, pia Chama cha Soka cha Ivory Coast kimeondoa utata kuhusu Kocha Francois Zahoui kwa kutamka ataiongoza Nchi hiyo hadi mwishoni mwa Agosti.
Mkataba wa Zahoui na Ivory Coast ulimalizika Mwezi Machi na wengi walitegemea ndio mwisho wake hasa baada ya kusakamwa na Viongozi wa Soka, Mashabiki na baadhi ya Wachezaji baada ya kufungwa kwenye Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa huko Nchini Gabon na Equatorial Guinea mwanzoni mwa Mwaka na Zambia kuifunga Ivory Coast na kutwaa Ubingwa.
Ivory Coast wanatarajiwa kucheza Mechi ya kujipima nguvu Jumapili na Mali huko Ufaransa na wenzao wa Tanzania wanacheza Jumamosi na Malawi Mjini Dar es Salaam.
RATIBA KUNDI C:
01-05/06/12: Ivory Coast v Tanzania
01-05/06/12: Gambia v Morocco
08-12/06/12: Morocco v Ivory Coast
08-12/06/12: Tanzania v Gambia
22-26/03/13: Ivory Coast v Gambia
22-26/03/13: Tanzania v Morocco
07-11/06/13: Gambia v Ivory Coast
07-11/06/13: Morocco v Tanzania
14-18/06/13: Tanzania v Ivory Coast
14-18/06/13: Morocco v Gambia
06-10/09/13: Ivory Coast v Morocco
06-10/09/13: Gambia v Tanzania
No comments:
Post a Comment