MSHAMBULIAJI Felix Sunzu kutoka Zambia jana aliipaisha Simba na kuiwezesha kufuzu kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Urafiki baada ya kuifungia bao pekee na la ushindi dhidi ya Karume Boys.
Sunzu alirejea nchini na kujiunga na timu hiyo juzi akitokea kwao Zambia alikokwenda kwa mapumziko baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.
Mshambuliaji huyo mrefu alifunga bao hilo dakika ya 58 baada ya kufanyika shambulizi kali kwenye lango la Karume Boys. Pambano hilo lilichezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyochezwa jana jioni, Azam iliichapa Mafunzo mabao 3-2. Wafungaji wa mabao ya Azam walikuwa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ dakika ya sita, Kipre Tchetche dakika ya 37 na Ibrahim Mwaipopo dakika ya 83.
Mafunzo ilijipatia mabao yake kupitia kwa Mohamed Abdulrahman dakika ya 46 na Jaku Joma dakika ya 62.
Kwa matokeo hayo, Simba imemaliza kinara wa kundi A ikiwa na pointi zake saba, ikishinda mechi mbili na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi tano, baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare mbili. Mafunzo imeaga michuano hiyo bila ya kuambulia pointi.
No comments:
Post a Comment