KLABU ya Arsenal inakaribia kumpata kwa mkopo kiungo wa klabu ya Real Madrid Nuri Sahin ili kuziba pengo la Alex Song ambaye amesajiliwa na Barcelona. Sahin mwenye umri wa miaka 23 ambaye pia alikuwa akiwindwa na klabu ya Liverpool katika kipindi hiki usajili anatarajiwa kujiunga na Arsenal kwa msimu mzima wa Ligi Kuu huku kukiwa na uwezekano wa kumchukua moja kwa moja. Klabu hiyo inatarajiwa kutangaza ujio wa mchezaji huyo ambaye ni raia wa Uturuki baadae wiki hii ili kuziba pengo la Song ambaye amekwenda Barcelona kwa uhamisho wa paundi milioni 15.Sahin ambaye alijiunga na mabingwa hao wa Hispania akitokea klabu ya Borussia Dortmund kwa mkataba wa miaka sita aliosaini Mei mwaka 2011 ameshindwa kuonyesha cheche kutokana na majeraha ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakimwandama. Meneja wa Liverpool Brandan Rodgers ambaye amewahi kufanya kazi chini ya kocha wa Real Madrid Jose mourinho wakati akiinoa Chelsea naye alikuwa na matumaini ya kumpata Sahin ili kuongeza nguvu katika kikosi chake.
FEDERER ANYAKUWA TAJI LA CINCINNATI.
MCHEZA tenisi nyota kutoka Switzerland, Roger Federer amefanikiwa kumfunga Novak Djokovic wa Serbia katika mchezo wa fainali ya michuano ya wazi ya Cincinnati na kufanikiwa kunyakuwa taji hilo kwa mara ya tano. Federer ambaye ni bingwa wa michuano ya Wimbledon alimfunga Djokovic kwa 6-0 7-6 9-7 na kufanikiwa kunyakuwa taji hilo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Federer amesema kuwa amefurahi kushinda taji hilo na anajiona yuko katika kiwango bora kwa ajili ya michuano ya wazi ya Marekani inayotarajiwa kuanza Agosti 27 mwaka huu jijini New York. Federer mwenye umri wa miaka 31 ambaye alifungwa na Andy Murray katika michuano ya Olimpiki, sasa anakuwa ameshinda mataji sita ya ATP kwa mwaka huu. Kwa upande wa wanawake Li Na wa China alifanikiwa kunyakuwa taji hilo kwa kumfunga Angelique Kerber wa ujerumani kwa 1-6 6-3 6-1 likiwa ni taji lake la sita la michuano ya WTA.
No comments:
Post a Comment