BUKOBA SPORTS

Wednesday, August 15, 2012

FAMILIA YA MAFISANGO YATUPIWA VYOMBO NJE... NINI HATIMA YAKE?


Samani za aliyekuwa mchezaji wa Simba Marehemu Patrick Mafisango zikiwa nje ya nyumba aliyokuwa akiishi maeneo ya Chang’ombe Dar es Salaam baada ya mwenyenyumba kuvutoa kutokana na kudai kodi. Kulia ni pichani ndugu wa marehemu aliyekuwa akiishi na marehemu. Vyombo vya aliyekuwa kiungo wa Simba, marehemu Patrick Mafisango, jana vilitolewa nje kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na ndugu zake, Keko jijini Dar es Salaam. Ndugu wa Mafisango aitwaye Joel Mafisango ndiye alikuwa akiishi kwenye nyumba hiyo hata alipofariki kaka yake, ambapo jana vyombo vilitolewa nje kutokana na kilichodaiwa kuwa mkataba ulimalizika na mwenye nyumba aitwaye Chingweni Mtoro.
Joel alisema kitendo kilichofanywa na uongozi wa Simba kuacha hadi kufukuzwa kwenye nyumba si kizuri kwani walikuwa wanataka kuuza vifaa hivyo ili warudi kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini walizuiwa  na uongozi wa klabu hiyo kwa kueleza wataendelea kulipa kodi hiyo. 
"Tulichofanyiwa na Simba, tunaimani kuwa wametuonea kwa sababu tulikuwa na mpango wa kuuza vyombo vya ndugu yetu ili tupate nauli, lakini walitukataza sasa wametuacha tunateseka," alisema.
Naye mwenye nyumba hiyo, Mtoro alisema Julai 28 mwaka huu ilikuwa mwisho wa mkataba wa marehemu Mafisango, ingawa Simba ilimtuma mdau wake mmoja ikaomba ipewe muda zaidi ili uongozi uendelee kujipanga lakini hadi sasa imeshindikana.
"Fedha ambazo zinatakiwa kulipwa kwa ajili ya pango ni Sh 350,000 kwa mwezi. Kwa sasa mimi nimeshapata mpangaji mpya hivyo ninalazimika kuwaondoa ili aingie kwani ana shida na nyumba lakini niseme kwa ukweli kwamba nilitumia taratibu zote zinazostahili," alisema Mtoro. 
Akizungumzia hilo Makamu  Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alikiri kwamba  mkataba wa pango kwenye nyumba hiyo umeisha na kuwataka ndugu hao kurejea kwao kama hawana kazi ya kuwawezesha kuishi.
"Tunaweza kuwasaidia lakini si wajibu wetu, notisi ilitoka na kati ya hao mmoja ambaye ni ndugu wa Mafisango, alikwenda hadi Kinshansa kuzika ila wengine ni ndugu wa kuungaunga. 
"Huyo wa Kinshasa ambaye ni ndugu wa marehemu tutampa nauli kama akiwa tayari kwa muda wake. Tatizo hawataki kurudi kwao na wanataka Simba iwape nyumba na fedha ya chakula je yanawezekana hayo? Alihoji Kaburu.

No comments:

Post a Comment