BUKOBA SPORTS

Thursday, October 4, 2012

BRAZIL YAENDELEA KUBAKIA NJE YA KUMI BORA ORODHA ZA FIFA.

NCHI za Ulaya zimeendelea kutamba katika orodha za juu za ubora zinazotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA huku Hispania ikiendelea kuwa king’ang’anizi na kubakia katika nafasi ya kwanza katika orodha hizo huku Tanzania ikibakia katika nafasi yake ya 132 waliyokuwepo mwezi uliopita. Nafasi ya pili inashikiliwa na Ujerumani huku nafasi ya tatu ikishikwa na Ureno ambao wamepanda kwa nafasi moja, nafasi ya nne inashikiliwa na Argentina ambao wamepanda kwa nafasi tatu na tano bora inafungwa na Uingereza ambao mwezi uliopita walikuwa nafasi ya tatu. Nafasi ya sita inashikiliwa na Uholanzi ambao wamepanda nafasi mbili, Uruguay wako katika nafasi ya saba wakiwa wameporomoka nafasi mbili huku Italia nao wakidondoka mpaka nafasi ya nane kutoka ya sita waliyokuwa mwezi uliopita. Colombia ambao mwezi uliopita walikuwa katika nafasi ya 22 wamepaa mpaka nafasi ya tisa na 10 bora inafungwa na Ugiriki ambao wamepanda nafasi moja wakati mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia Brazil bado wanasuasua baada ya kuanguka kwa nafasi mbili mpaka ya 14. Kwa upande wa tano bora ya Afrika nafasi ya kwanza bado inashikiliwa na Ivory Coast ambao wako nafasi ya 16, nafasi ya pili inashikiliwa na Algeria ambao wamepanda kwa nafasi nne mpaka ya 24, nafasi ya tatu wapo Mali ambao wamepanda kwa nafasi tano mpaka nafasi ya 27. Nafasi ya nne inashikiliwa na Misri wakiwa wameporomoka mpaka nafasi tatu mpaka ya 40 wakati mabingwa wa Afrika Zambia ndio wanakamilisha tano bora ya Afrika wakiwa katika nafasi ya 41.

No comments:

Post a Comment