WASHIRIKI wa fainali za taifa za mashindano ya urembo nchini mwaka huu 'Redd's Miss Tanzania 2012' kila mmoja ametamba kuibuka na ushindi katika shindano hilo lililopangwa kufanyika Novemba 3 kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kambini kwao katika hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam leo idadi kubwa ya warembo hao kutoka kanda mbalimbali nchini wamemtaja mrembo wa taifa wa shindano hilo mwaka 2005, Nancy Sumary kuwa ndiye mfano wa kuigwa katika sanaa hiyo kutokana na tabia aliyonayo ya kujiheshimu na kujitambua.
Noela Michael (19) ambaye ni mrembo wa kitongoji cha Tabata na Kanda ya Ilala jijini alisema kuwa amejiandaa vizuri ili kuendeleza rekodi iliyowekwa na warembo wengine wa kanda hiyo kutwaa hilo kwa kushinda taji linaloshikiliwa na mrembo wa Ilala, Salha Israel.
Noela alisema kuwa mbali na kuwa mshindi wa taji hilo yeye ni mrembo anayejitambua na anayetaka kuipa thamani sanaa hiyo ambayo baadhi ya wazazi wanaipinga kutokana na kuwafanya mabinti zao kujiingiza kwenye tabia zisizokubalika katika jamii.
"Ila nitakubaliana na matokeo kwa sababu naamini mshindi ni mmoja na atakapotangazwa, waliobakia si kwamba ni wabaya," alisema Noela.
Mrembo kutoka Temeke, Edda Sylivester (21) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu Mlimani alitamba naye anajiamini na amejipanga kufanya vizuri kwenye shindano hilo na hatimaye kwenye mashindano ya urembo ya Dunia.
Edda aliwataka warembo walio na dhana ya kuona sanaa hiyo haijengi wabadilike na kuamini kuwa hiyo ni moja ya kazi zinazoweza kumjenga msichana kutokana na kuandaliwa vyema katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.
"Nataka kufuata nyayo za Nancy, naamini mie ndiyo Miss Tanzania wa mwaka huu na nitaipeperusha vyema bendera ya nchi," alisema mrembo huo ambaye pia ni Miss Kigamboni.
Belinda Mbogo (21) kutoka Kanda ya Kati alisema kuwa amejipanga kurejesha taji hilo la taifa mkoani Dodoma licha ya kuwepo na ushindani kwa washiriki wa fainali hizo.
"Nitafurahi kuona ndoto zangu zinatimia za kurejesha taji Dodoma, ni muda mrefu umepita tangu Emily Adolph alipotwaa taji hili," alisema mrembo huyo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Nancy ndiye mrembo aliyewahi kufanya vizuri katika shindano hilo ambapo alitwaa taji la umalkia wa Afrika na kuingia kwenye hatua ya sita bora ya dunia.
Washiriki hao wakiwa kambini wananolewa na Salha kwa kushirikiana na Irene Kyarugaba ambaye aliwahi kushiriki fainali zilizopita.
No comments:
Post a Comment