BUKOBA SPORTS

Monday, February 11, 2013

BAADA YA NIGERIA KUTWAA KOMBE RAIS WAO JONATHAN AIPONGEZA SUPER EAGLES.

RAIS wa Nigeria, Goodluck Jonathan amekipongeza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Super Eagles kwa kunyakuwa Kombe la Mataifa ya Afrika-Afcon baada ya kuifunga Burkina Faso kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana katika Uwanja wa Taifa jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Katika taarifa iliyotolewa ofisini kwake rais Jonathan alimshukuru kocha Stephen Keshi, wachezaji na viongozi wote ambao walifanya kazi ngumu kuifanya Super Eagles kupata ubingwa wa kujivunia baada ya miaka 19 kupita. Rais pia anaamini kwa ushindi huo waliopata katika Afcon itakuwa chachu ya mafanikio zaidi huko mbele hususani katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil mwakani. Jonathan aliishukuru serikali ya Afrika Kusini na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kwa maandalizi mazuri ya michuano hiyo na kuahidi kuwaandalia mapokezi makubwa Super Eagles pindi watakapotua jijini Abuja, Jumanne. Bao pekee lililoipa ushindi Super Eagles na kukata kiu yao ya miaka 19 ya kulikosa kombe hilo lilifungwa na mchezaji ambaye anacheza katika timu inayoshiriki Ligi Kuu nchini Nigeria Sunday Mba.Matokeo hayo pia yanamuingiza Keshi katika vitabu vya kumbukumbu akiwa kocha wa pili kushinda kombe hilo akiwa kama mchezaji na baadae kocha, wa kwanza kufanya hivyo alikuwa marehemu Mahmoud El Gohary wa Misri.

No comments:

Post a Comment