Kipa wa Ghana, Fatau Dauda (kulia) na Kwadwo Asamoah wakilinda goli lao huku Prejuce Nakoulma wa Burkina Faso akijaribu kufunga wakati wa mechi yao ya nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwenye Uwanja wa Mbombela mjini Nelspruit jana Februari 6, 2013. Picha: REUTERS
Wachezaji wa Ghana wakiwa hoi baada ya kupoteza mechi yao ya nusu fainali ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Mbombela mjini Nelspruit jana Februari 6, 2013. Burkinabe walishinda kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1. Picha: REUTERS
Wachezaji wa Ghana wakiwa hoi baada ya kupoteza mechi yao ya nusu fainali ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Mbombela mjini Nelspruit jana Februari 6, 2013. Picha: REUTERS
REFA Mtunisia Slim Jdidi amefungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufuatia maamuzi ya utata katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika juzi baina ya Burkina Faso na Ghana.
"CAF haijafurahishwa na kiwango cha uamuzi katika mechi ile," katibu mkuu Hicham El Amrani aliviambia vyombo vya habari.
"Tunajua kwamba wanaweza kufanya makosa lakini tunatarajia kiwango kizuri zaidi cha uamuzi. Wanawekewa viwango kulingana na kila mechi waliyochezesha na kulingana na maksi zake, refa kutoka Tunisia sasa amefungiwa kwa muda ambao bado haujaamuliwa."
Miongoni mwa matukip ya utata katika mechi ya jana mjini Nelspruit yalikuwa ni kumpa kadi nyekundu mshambuliaji wa Burkina Faso, Jonathan Pitroipa ambayo huenda ikamfanya akakosa mechi ya fainali dhidi ya Nigeria Jumapili.
Pitroipa alionyeshwa njano ya pili katika mechi hiyo kwa kujiangusha ndani ya eneo la penalti, katika dakika 30 za nyongeza.
Kamati ya maandalizi itaamua kesho Ijumaa kama mchezaji huyo atacheza mechi ya fainali.
Burkina Faso wamekata rufaa lakini El Amrani alisema namna pekee ambayo Pitroipa atanusurika adhabu ya kutocheza mechi moja ni kama tu refa Jdidi aliandika katika ripoti yake kwamba alifanya makosa.
"Kamati ya maandalizi haina nguvu kubadili maamuzi ya refa," El Amrani alifafanua.
"Kama refa alikiri kwamba alifanya makosa katika ripoti yake kamati italizingatia na kufanya maamuzi yoyote kama ni muhimu. Lakini ripoti ile.... ndiyo ya mwisho."
Jdidi pia aliwapa penalti "nyepesi mno" Ghana katika maamuzi ambayo yangeweza kuwa mjadala mkubwa zaidi wa mechi hiyo ya kuvutia ambayo Burkina Faso hatimaye walishinda kwa penalti 3-2 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 1-1.
No comments:
Post a Comment