MADRID, Hispania
WINGA wa zamani wa Tottenham Hotspur, Gareth Bale, aliyesajiliwa msimu huu katika kikosi cha Real Madrid kwa dau la rekodi ya dunia, amefanikiwa kupata nyumba mpya ya kupanga Madrid ambayo atakuwa akilipa kodi ya euro 10,000 (sh milioni 21.251) kwa mwezi.
Bale mwenye umri wa miaka 24, alisema kuwa anajisikia furaha kukaa katika Jumba hilo lililopo karibu na mjengo wa Cristiano Ronaldo, aliyevunja rekodi yake ya kusajiliwa.
“Wazazi wangu, Frank na Debora walikuja kunitembelea hapa wakiwa pamoja na mchumba wangu, Emma Rhys-Jones na mtoto wetu Alba, hii ni hatua nzuri kwangu na ninafurahia kuwa katika kikosi hiki,” alisema Gareth.
Mchezaji huyo ameingia mkataba wa miaka sita wenye thamani ya kitita cha euro milioni 100, baada ya kukamilika kwa mchakato mrefu wa usajili huo na kuongeza chachu ya safu ya ushambuliaji ya Santiago Bernabeu.
@@@@@@@@
Gerrard atamani ukocha Liverpool LIVERPOOL, England
NAHODHA wa Liverpool, Steven Gerrard amesema kuwa amebakiza muda mfupi wa kuitumikia klabu hiyo uwanjani na sasa anatamani kuwa mmoja wa makocha wa klabu hiyo, mara baada ya kutundika daluga.
Gerrard (33), alisema kwamba anamapenzi makubwa na timu hiyo, hivyo amewaomba viongozi wake walifikirie suala hilo ili aendelee kuitumikia Liverpool katika maisha yake yote.
“Ndoto zangu ni kuwa kocha wa Liverpool mara nitakapostaafu soka. Kwangu ni fahari kubwa kuitumikia klabu hii ambayo nina mapenzi nayo ya dhati,” alisema Gerrard na kuongeza kuwa:
“Ukiona umefikia umri wa kutaka kustaafu soka, ni lazima uanze kufikiria mambo makubwa kwa ajili ya maisha ya baadaye, hivyo mikakati yangu ni kuwa meneja wa timu hii.”
@@@@@@@@@
Messi aibeba Barca, aumia mguu BARCELONA, Hispania
STRAIKA wa Barcelona, Lionel Messi usiku wa kuamkia jana alifanikiwa kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Almeria, lakini alijikuta anashindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia mguu wake wa kulia.
Messi, ambaye Ijumaa iliyopita alitinga mahakamani kujibu mashitaka yanayohusiana na ukwepaji wa kodi, alifunga bao dakika ya 21 likiwa ni la 11 msimu huu katika mashindano yote.
Adriano Correia aliongeza bao la pili na la ushindi kwa timu hiyo. Kuumia kwa nyota huyo kumemsikitisha Kocha wake, Gerardo Marino kwa kile alichodai kuwa, mwanandinga huyo ni muhimu katika kikosi chake.
“Kuumia kwa Messi ni pigo kubwa kwetu kwa sababu ni muhimu sana katika timu hii na sasa nawaachia madaktari ambao watamfanyia vipimo ili kujua ameumia kwa kiasi gani ila kwa sasa siwezi kusema chochote,” alisema Marino.
No comments:
Post a Comment