Kikosi cha Yanga kilichoanza kucheza na Kagera Sugar leo Jumamosi
Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo kati ya wenyeji, Kagera Sugar na Yanga SC umeingiza kiasi cha Sh. Milioni 20. 5, wakati kila klabu imepata mgawo wa Sh. Milioni 4.9.Taarifa kutoka Chama cha Soka Kagera (KRFA) usiku huu, imesema kwamba jumla ya Sh 20, 525,000 zimepatikana na kila timu imepata Sh. 4,907,000.
Katika mchezo huo, ambao Yanga SC imeibuka na ushindi wa 2-1, Sh. 3,139,320 ni makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), gharama za Uwanja Sh. 2,495,000 na gharama za mechi Sh. 1,497,000.
Makato mengine ni mgawo wa Kamati ya Ligi Sh. 1,497,000, KRFA 582, 100 na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepata Sh. 748,543.
Mabingwa watetezi Yanga SC wamepata ushindi wa kwanza ugenini msimu huu baada ya kuilaza Kagera Sugar mabao 2-1, hivyo kupaa hadi nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 15, nyuma ya Simba SC yenye pointi 18.
Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili mfungaji Mrisho Ngassa aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kurushwa wa beki wa kulia Mbuyu Twite, kabla ya Kagera kusawazisha dakika ya 47 kupitia kwa Godfrey Wambura na Hamisi Kiiza kufunga la ushindi dakika ya 59.
No comments:
Post a Comment