BUKOBA SPORTS

Friday, December 13, 2013

WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO KUZINDUA TAMASHA LA VIPAJI.


Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya ukuzaji vipaji vya sanaa na muziki (Unscripted Concert for Africa-Tanzania, UCA-Tz), Emmanuel Mushy (katikati) akizungumza na waandishi wa habari juu ya tamasha la UCA-Tz litakalofanyika kesho jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kutoka kushoto ni Mwakilishi kutoka kampuni ya Zantel, Divine Mosi na Fadhil Nandonde kutoka UCA-Tz, kulia ni mwakilishi wa vijana kutoka nchini Uganda, Ms. Faridah Nalunkuma.

Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya ukuzaji vipaji vya sanaa na muziki (Unscripted Concert for Africa-Tanzania, UCA-Tz), Emmanuel Mushy (katikati) akizungumza na waandishi wa habari juu ya tamasha la UCA-Tz litakalofanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa vijana kutoka nchini Uganda, Ms. Faridah Nalunkuma akizungumza na waandishi wa habari juu ya uwakilishi wake wa UCA, na kuzungumzia tamasha kwa ujumla.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya ukuzaji vipaji vya sanaa na muziki (Unscripted Concert for Africa-Tanzania, UCA-Tz), Emmanuel Mushy alipozungumza nao juu ya tamasha la UCA-Tz litakalofanyika kesho jijini Dar es Salaam. PICHA ZOTE NA THEHABARI.COM

Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha la vipaji vya sanaa na muziki lililoandaliwa na asasi ya ukuzaji vipaji (Unscripted Concert for Africa-Tanzania, UCA-Tz).
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo, Emmanuel Mushy alisema tamasha hilo la pekee litakalofanyika Uwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam linatarajia kushirikisha vijana zaidi ya 500 kutoka maeneo anuai ya jiji.

Akifafanua zaidi juu ya tamasha hilo, Mushy alisema UCA-Tz ni program yenye dhumuni la kutoa nafasi kwa vijana wenye vipaji vya muziki na sanaa ili vijana hao waweze kukua katika vipaji vyao.
“…Neno ‘unscripted’ linamaanisha kitu ambacho kipo lakini hakijaandikwa, yaani kwa maana nyingine ni kitu kilichopo nyuma ya pazia. UCA-Tz baada ya utafiti imebaini kuwa kuna vijana wengi ambao wanajihusisha na muziki pamoja na sanaa lakini hawapati ile nafasi (platform) ya kuendeleza vipaji vyao, hivyo ni kama vijana hawa wapo nyuma ya pazia,” alisema Mushy.

Aliongeza kuwa UCA Tz kwa kutambua umuhimu wa vipaji vya vijana vinavyopotea imeona umuhimu wa kutengeneza njia kwa vipaji hivyo ili vitoke nyuma ya pazia kukua na hatimaye kujionesha kwa jamii. Aidha alisema moja ya njia ambazo UCA-Tz inazifanya ni kuandaa matamasha ya vipaji kwa kila mwaka kuwashirikisha vijana na kwa mara ya kwanza inazindua Tamasha la vipaji nchini Tanzania, ambalo litashirikiza vijana zaidi 500 kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

“…Tamasha hili la vipaji linatarajia kufanyika kesho, Jumamosi ya tarehe 14th December pale Uwanja wa Kinondoni Biafra, kuanzia saa 7 mchana hadi saa 12 za jioni. Katika tamasha hilo vijana wenye vipaji vya kuimba, ku-rap, kucheza, kuchora na ubunifu (ku-design) watawasilisha kazi zao kwa umati utakao jitokeza na vijana wenzao,” alisema Mushy.

Alisema ili kuleta radha na hamasa zaidi asasi hiyo imealika wawakilishi vijana kutoka nchi mbalimbali za Africa kama Kenya, Uganda na Ghana ambao nao watashiriki. “…Kutakua na outside performances kutoka kwa wasanii mbalimbali ambao wameshapiga hatua kwenye tasnia za muziki na sanaa nao watashiriki kwa pamoja.

Naye Mwakilishi kutoka kampuni ya Zantel, Divine Mosi ambao ni moja wa makampuni yaliofanikisha tamasha hilo, akizungumza alisema kampuni yao itaendelea kuunga mkono shughuli anuai za kuwawezesha vijana ikiwa ni sehemu ya kurudisha mchango wa wateja wao wanaotumia mtandao wao.

Kampuni nyingine zilizounga mkono kiushirikiano (supporters/sponsers) kufanikisha tamasha hilo ni pamoja na kampuni ya Coca Cola, Maezeki, Arise Media, LGBY Media na mtandao wa kijamii wa habari-Thehabari.com (www.thehabari.com) na mitandao mingine ya kijamii nchini.

No comments:

Post a Comment