STRAIKA wa Mabingwa wa Dunia Spain na Atletico Madrid, ambao ni Mabingwa wa Spain, Diego Costa, amefuzu upimwaji afya yake huko Chelsea akiwa njiani kukamilisha Uhamisho unaokadiriwa kugharimu Pauni Milioni 32.
Chelsea imeafika kulipa Dau ambalo linatajwa kwenye Mkataba wa Diego Costa na Atletico ikiwa atahama kabla muda kwisha na sasa amebakiza kuafikiana na Chelsea kuhusu marupurupu yake binafsi ili akamilishe Uhamisho.
Msimu huu, Costa, mwenye Miaka 25, alifunga Bao 36 katika Mechi 52 alizochezea Atletico na kuiwezesha kutwaa Ubingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza tangu 1996 na pia kuifikisha Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI walikonyukwa Bao 4-1 na Real Madrid.
Costa, Mzaliwa wa Brazil, hivi sasa yupo na Kikosi cha Spain ambacho kinajiandaa kwenda kutetea Taji lao huko Brazil kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Mwezi Mei, Meneja wa Chelsea, Jose Mourinho, alilalamika kwa kumkosa ‘Straika Muuaji’ na akatangaza kutoa kipaumbele kumnasa Straika wa aina hiyo kabla Msimu ujao haujaanza.
Msimu huu, Chelsea ilifunga Bao 71 tu na kupitwa kwa Bao 31 na Mabingwa Manchester City huku Mastraika wa Chelsea, Samuel Eto'o, Fernando Torres na Demba Ba, wakifunga jumla ya Bao 19 tu na Eto’o, ambae sasa amemaliza Mkataba na Chelsea, akifunga Bao 9.
Kwenye La Liga, Costa alifunga Bao 27 akiwa Nafasi ya 3 kwenye Ufungaji Bora nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, Bao 31, na Lionel Messi wa Barcelona, Bao 28.
No comments:
Post a Comment