BUKOBA SPORTS

Monday, December 8, 2014

FALCAO FITI SASA KUCHEZA KWA MUDA!

MENEJA wa Manchester United Louis van Gaal amesema hajali ikiwa Radamel Falcao ananung’unika kupigwa Benchi kwa vile yuko fiti kucheza Dakika 20 tu za Mechi.
Tangu atue Man United kwa Mkopo kutoka AS Monaco mwanzoni mwa Msimu huu, Falcao hajawahi kumaliza Mechi nzima huku akikumbwa na maumivu ya mara kwa mara.
Falcao, ambae mwanzoni mwa Mwaka aliumia vibaya Goti lililomfanya akose kuichezea Nchi yake Colombia kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil, hivi karibuni alikuwa nje kwa Wiki 6 akiwa na tatizo la Musuli lakini alirejea kwa Mechi mbili zilizopita za Man United akiwekwa Benchi.
Van Gaal amemuonya Falcao kuwa hataanza Mechi hadi hapo atakapokuwa fiti kabisa.
Alipohojiwa na Wanahabari kama anahisi Falcao anafurahia kuwa Benchi, Van Gaal alijibu: “Sijali hilo. Lazima afuate falsafa yangu..unaelewa? Nipo hapa kwa hilo!”
Van Gaal alifafanua kuwa ili kurejea Timu ya Kwanza Falcao aliwajibika kucheza Mechi Kikosi cha Pili lakini alilazimika kumweka Benchi Jumanne iliyopita kwenye Mechi na Stoke City kwa sababu Wayne Rooney alikuwa kaumia.

No comments:

Post a Comment