BUKOBA SPORTS

Friday, January 29, 2016

BONANZA LA MICHEZO KWA SHULE ZA MSINGI LA JAMBO BUKOBA LAFANA KATIKA VIWANJA VYA GYMKHANA BUKOBA MANISPAA

Bw. Clemence N. Mulokozi mwazilishi wa shirika la Jambo Bukoba akiteta Jambo leo hii wakati wa Bonanza hilo.

Shirika la Jambo Bukoba lisilo la Serikali linalojihusisha na maendeleo ya elimu na michezo Mkoani Kagera limefanya Bonanza la michezo kwa shule za Msingi kutoka Halmashauri zote za Wilaya na Manispaa ya Bukoba lilofanyika 29 Januari, 2016 katika viwanja vya Gymkhana Manispaa ya Bukoba.
Katika Bonanza hilo Bw. Clemence N. Mulokozi mwazilishi wa shirika hilo wakati wa ufunguzi alisema Jambo Bukoba imekuwa ikijihusisha na mambo makuu manne ambayo ni kujenga miundombinu shuleni kama vyoo, Kuzisaidia shule katika upatikanaji wa vitabu, Kuzisaidia shule katika upatikanaji wa vifaa vya michezo na kutoa elimu ya UKIMWI kupitia michezo, na Kukarabati madarasa na ofisi za walimu katika shule.

Bw. Clemence aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Kagera kwa ushirikiano wanaoupata shirika la Jambo Bukoba katika kutekeleza majukumu yake aidha, aliwaomba wazazi kujitoa kushiriki katika kuwasaidia watoto wao katika upatikanaji wa uji na chakula shuleni ili watoto wacheze kwa afya njema na kushiriki kikamilifu katika masomo yao.
Mgeni rasmi katika Bonanza hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella ambaye katika hotuba yake alilipongeza sana Shirika la Jambo Bukoba kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Mkoa wa Kagera pia aliwashukuru wafadhili kutoka Ujerumani kwa kufadhili Jambo Bukoba Mkoani Kagera.
Mhe. Mongella alisema kuwa michezo inasaidia sana watoto kuchangamsha akili yao katika masomo darasani jambo ambalo linapelekea watoto hao kufaulu mitihani yao ya kawaida na ya mwisho katika kuhitimu elimu ya msingi tofauti na kutocheza ambapo watoto hukaa wamezubaa na kutochangamka na kupelekea akili kudumaa.
Mkuu wa Mkoa Mongella alitoa agizo kwa Maafisa Elimu kupitia kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya kuhakikisha wanatenga viwanja vya kuchezea watoto katika shule , kunnuua vifaa vya michezo na kutoa taarifa za michezo kwa Afisa Elimu Mkoa katika taarifa ya kila mwezi ya maendeleo ya elimu kwa kila Wilaya.
Aidha, Mhe Mongella aliliomba Shirika la Jambo Bukoba kushirikiana na Maafisa Elimu wa Wilaya na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kuendesha vikao vya wadau katika kila shule ili kuwa na uelewa wa pamoja wa michezo katika Mkoa na kushirikisha shule nyingi zaidi kuliko ilivyo sasa shule moja kila Wilaya.
Mwisho Mhe. Mongella aliwahakikishia Jambo Bukoba kuwa watapata kiwanja kikubwa cha kujenga shule au kituo cha michezo kwa ajili ya kufundishia michezo kwa watoto na watu wazima kucheza michezo mbalimbali katika Mkoa wa Kagera kama walivyoomba kwa uongozi wa Mkoa na alisema kiwanja hicho kitapatikana kabla ya Machi 1, 2016.
Bonanza hilo lilihusisha wananfunzi wanamichezo 240 kutoka katika shule za Msingi nane, wanafunzi 30 kila shule moja kutoka kila Halamashauri, wanafunzi hao wavulana 15 na wasichana 15 waliwakilisha kila Halmashauri wakiwa na walimu wawili wawili kutoka kila shule bingwa ngazi ya Wilaya.
Aidha, shule zilizoshiriki katika Bonanza hilo zilipatikana kutoka kila Halmashauri kwa kuendesha mabonanza ya Wilaya na shule washindi ndiyo waliowakilisha shule nyingine katika kila Wilaya. Shule hizo ni Kaagya (Halmashauri ya Wilaya Bukoba), Iteera (Kyerwa), Ibuga (Muleba), Mafumbo (Manispaa ya BUkoba), Murusagamba (Ngara), Mwemagea (Missenyi), na Maguge (Karagwe).
Washindi waliopatikana katika mashindano ya bonanza la Mkoa wamezawadiwa shilingi 4,000,000/= kila shule na fedha hizo zitatumika katika kuimarisha miundombinu ya shule husika kama kujenga matundu ya vyoo, kukarabati madarasa na ofisi za walimu kwa kushirikiana na jamii ya eneo husika.
Shirika la Jamboa Bukoba mwanzilishi wake ni Bwana Clemence N. Mulokozi ambaye Baba yake ni mzaliwa wa Ishozi Wilayani Missenyi na mama yake ni Mjeurumani.

No comments:

Post a Comment