BUKOBA SPORTS

Wednesday, February 24, 2016

FULL TIME: KOMBE LA SHIRIKISHO, YANGA 2 v 1 JKT MLALE, NONGA NA KAMUSOKO WAIPELEKA YANGA ROBO FAINALILEO TAIFA!


YANGA imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la FA baada ya kuifunga JKT Mlale mabao 2-1 hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.
Mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wachache ulifanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambapo hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.

Bingwa wa Kombe la FA atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mwakani.
Ikicheza huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoupata Jumapili kutoka kwa mahasimu wao Simba, Yanga ilianza kwa kasi kushambulia lango la wapinzani wao, lakini umaliziaji haukuwa mzuri.
Baada ya mashambulizi ya kila upande, JKT Mlale iliypo Ligi Daraja la Kwanza, iliandika bao la kuongoza dakika ya 21 mfungaji akiwa Mgandila Shaaban baada ya kuunganisha pasi ya Said Ngapa.
Yanga nusura ipate bao la kusawazisha dakika ya 34 baada ya mpira wa Simon Msuva kugonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa JKT Mlale.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika ya 42 Paul Nonga aliisawazishia Yanga bao akiunganisha krosi ya Godfrey Mwashiuya.
Kipindi cha pili Yanga ilimtoa Matheo Simon na kumuingiza Donald Ngoma, huku pia ikimtoa Salum Telela aliyeumia na kumuingiza Thabani Kamusoko.
Mabadiliko hayo yaliisaidia zaidi Yanga, ambapo dakika ya 58 Kamusoko alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi ya Mwashiuya.
Michuano hiyo iliyoshirikisha timu 64 kutoka ngazi za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, ambayo jana ilianza hatua ya 16 bora itaendelea tena kesho kwa michezo miwili.
Michezo hiyo ni Ndanda FC dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, huku Coastal Union wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Jumamosi Mwadui FC watawakaribisha Rhino Rangers katika uwanja wa Mwadui Complex - Shinyanga, ambapo Jumapili Simba SC itacheza na Singida United Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Mchezo mwingine siku hiyo ni Panone FC itakuwa mwenyeji wa Azam FC Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, huku Toto African wakicheza na Geita Gold Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

No comments:

Post a Comment