BUKOBA SPORTS

Tuesday, September 20, 2016

MAN UNITED – NINI KIMEENDA MRAMA? MOURINHO, ROONEY, POGBA, MFUMO AU MAJANGA TU?

WALIANZA vyema Msimu huu chini ya Meneja Mpya Jose Mourinho kwa kubeba Ngao ya Jamii na kisha kushinda Mechi zao 3 za EPL lakini Wiki moja iliyopita Manchester United wakafungwa na Man City, kisha Alhamisi kuchapwa na Feyenoord kwenye UEFA EUROPA LIGI na Jumapili kupigwa na Watford.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mourinho kupigwa Gemu 3 mfululizo akiwa Meneja tangu Agosti 2006 alipokuwa Chelsea.
Vipigo hivyo vya Mechi 3 mfululizo vimezua maoni tofauti kutoka kwa Wachambuzi huko England huku kila mmoja akitoa nadharia yake.
Wapo wanaodai kuwa hadi sasa Mourinho hajajua kupanga Kikosi cha Kwanza cha Man United wakihoji kuchezeshwa kwa Henrikh Mkhitaryan na Jesse Lingard kwenye kipigo cha City wakiwa ndio kwanza tu wametoka kwenye Majeruhi huku Marcus Rashford akipigwa Benchi licha ya kupiga Mabao kwenye Mechi na Hull City na alipoichezea England U-21.

Kwenye Mechi hiyo, Rashford na Ander Herrera waliingizwa baada ya Mapumziko na kubadilisha kabisa Gemu na City kuponea chupuchupu.
Kwenye kipigo cha Watford, Wachambuzi walimhoji Mourinho kuutosa Mfumo wake wa kawaida wa 4-2-3-1 na kutumia 4-3-3 ambao Paul Pogba alicheza Kiungo wa Kushoto na Wayne Rooney Kiungo wa Kulia wakati Mourinho mwenyewe alidai Rooney si Kiungo bali ni Namba 10, 9 au 9½!
Wote, Pogba na Rooney, walivurunda kwenye Mechi hiyo.
Wapo wanaohoji uchezaji wa Pogba, ambae alilipiwa Pauni Milioni 89.3 kwenye Uhamisho likiwa Dau la Rekodi ya Dunia, na kumtaka Mourinho abuni Mfumo utakaoenda na uchezaji wa Pogba.
Hao wanamtaka Mourinho kumpanga Kiungo Michael Carrick, nyuma ya Pogba, kwani ni mbunifu na Mfumo huo utakopi ule wa Juventus ambako Lejendari Andrea Pirlo, mpishi wa mashambulizi yote, alicheza Kiungo nyuma ya Pogba, na kumwacha Kiungo huyo Kijana wa France kuranda kote Kati na kusakama Goli la Wapinzani.
Lakini pia Wachambuzi hao wanamtaka Mourinho kuwa mkali na kummwaga Staa yeyote ambae hana mchango kwa Timu.

Kwa hilo, kidole kilichokomaa, kimewalenga Kepteni Wayne Rooney, Zlatan Ibrahimovic, Marouane Fellaini na hata Pogba ambae Lejendari wa Man United, Paul Scholes, amedai Kijana huyo anajidai Lionel Messi kwa kutaka kuwapiga chenga Wachezaji Wapinzani Watatu au Wanne wakati akicheza badala ya njia rahisi ya kutoa pasi za haraka na sahihi kwa wenzake ili kuzifungua kirahisi Difensi za Wapinzani.

Hata hivyo, Wachambuzi hao hao wanadai huwezi kuusahau mchango wa Ibrahimovic wa Bao 4 katika Mechi 5 za Ligi.

Mwenyewe Mourinho amekiri: “Tulianza Msimu vizuri, pengine ni mwanzo mzuri mno kwa Meneja mpya wa Man United kuliko wote lakini sikuwaza kwamba Timu iko tayari, haifungiki. Hapana kabisa!”

“Nilijua zipo kasoro, Wachezaji wengi wakiwa hawajafikia kilele cha ubora na wanafanya makosa!”

Lakini pia Mourinho amelalamikia kuadhibiwa kwa makosa kadhaa ya Marefa yaliyochangia mno kufungwa hizo Mechi zao 3.
Mourinho ametoboa Bao la kwanza la Watford halikupaswa kuwepo kwani Anthony Martial aliporwa Mpira kwa Rafu wakati kwenye Mechi na Man City walinyimwa Penati 2 na kile kipigo cha 1-0 cha Feyenoord kilitokana na Bao la Ofsaidi.
Mourinho ameeleza: “Makosa makubwa ya Marefa yapo nje ya uwezo wangu, sina lolote la kufanya. Tumeadhibiwa kwa makosa hayo na siwezi kufanya lolote!”
Jumatano Usiku, ndani ya Sixfields Stadium, Man United wana nafasi murua ya kuleta mabadiliko ya haraka watakapocheza na Northampton Town Mechi ya Raundi ya 3 ya EFL CUP, Kombe la Ligi.
Je, Jose Mourinho ataleta mapinduzi na kuliibua upya Jahazi la Old Trafford linaloenda mrama?

No comments:

Post a Comment