MANCHESTER City sasa wameruhusiwa kumtumia Staa Mbrazil wa Miaka 19 Gabriel Jesus kwenye Mechi yao ya EPL, Ligi Kuu England, ya kesho Jumamosi dhidi ya Tottenham Hotspur.
City walishafikia makubaliano na Klabu ya Brazil Palmeiras tangu Mwezi Julai Mwaka Jana kumnunua Kinda huyo wa Brazil mwenye Miaka 19 kwa Dau la Pauni Milioni 27 na pia kukubali Mchezaji huyo abakie Palmeiras hadi Msimu wa Brazil utakapoisha Mwezi Desemba. Jesus amekuwa Kambini na City kwa Wiki 3 sasa lakini ukiritimba umekwamisha Uhamisho wake kukamilika rasmi na hivyo kusitisha kuichezea rasmi City. Kinda huyo ndio kwanza amechomoza kwenye Soka la Dunia akiwa na Msimu wa Pili tu na Palmeiras lakini akaiongoza Klabu hiyo kutwaa Ubingwa wa Taifa Mwezi Novemba baada ya kutwaa Medali ya Dhahabu akiichezea Brazil kwenye Michezo ya Olimpiki, RIO 2016, Mwezi Julai.
Jesus alianza kukichezea Kikosi cha Kwanza cha Timu ya Taifa ya Brazil Mwezi Septemba Mwaka Jana na kufunga Bao 4 katika Mechi zake 6.
Hivi sasa Man City wapo Nafasi ya 5 kwenye EPL, wakiwa Pointi 10, nyuma ya Vinara Chelsea baada ya kufungwa Mechi 2 kati ya 3 walizocheza mwisho.
JE WAJUA?
-Jesus alijilukana kama Gabriel Fernando alipoanza kuichezea Palmeiras akiwa na Miaka 17.
-Akiwa huko alipewa Jezi Namba 33 [Umri wa Yesu Kristu] na mmoja wa Maafisa Habari wa Klabu hiyo akammwambia atumie Jina la Gabriel Jesus.
-Akiwa na Man City, Jesus pia atavaa Jezi Namba 33 ambayo awali ilivaliwa na Nahodha wa City Vincent Kompany.
No comments:
Post a Comment