BUKOBA SPORTS

Monday, April 23, 2018

TUMBAKU MORO, UCHUKUZI SC ZANG'ARA MEI MOSI

Kikosi cha timu ya soka ya Uchukuzi kikiwa pamoja na kocha wake Mkuu Zenno Mputa (kulia) na Mshauri wa timu Kennedy Mwaisabula (Mzazi), kinachoshiriki katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika katika viwanja mbalimbali mkoani Iringa. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).
Mshambuliaji Ramadhani Madebe (23 jezi nyekundu) wa Uchukuzi akiwa katika msitu wa wachezaji wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Joseph Mlimi (2), Mohamed Koshuma (16) na Stephen Mgendi (12) katika mchezo wa michuano ya Mei Mosi uliofanyika kwenye jana uwanja wa Samora. Uchukuzi walishinda bao 1-0. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).
Kipa Stanley Mwalega (aliyesimama kushoto golini) wa Tanesco akijiandaa kudaka mpira uliopigwa na Emmanuel Kiwea (2) wa timu ya Tumbaku ya Morogoro wakati wakicheza mchezo wa mechi ya Kombe la Mei Mosi ulifanyika leo kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Winga Salum Idd wa Tumbaku ya Morogoro (11) akikokota mpira kuelekea langoni mwa Tanesco wakati wa mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa. Tumbaku walishinda mabao 2-0. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).

Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU za Tumbaku ya Morogoro na Uchukuzi zinaongoza katika mchezo wa soka kwa kushinda kwenye michezo yao ya michuano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Iringa.
Tumbaku ipo katika kundi `A’ inaongoza kwa kuwa na pointi sita baada ya kushinda mechi mbili ikifuatiwa na timu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), RAS Iringa na Hifadhi ya Ngorongoro, ambazo zote hazina pointi.
Nayo Uchukuzi inaongoza kundi ‘B’ baada ya kushinda mchezo mmoja nakuwa na pointi tatu, wakifuatiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Geita Gold Mine (GGM) na NAO wote hawajakusanya pointi yeyote.

Katika hatua nyingine timu ya Tumbaku jana iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwafunga Tanesco magoli 2-0 katika mchezo uliofanyika leo kwenye uwanja wa Samora.

Washindi walipata bao lao la kwanza katika dakika ya 22 kwa njia ya penati lililofungwa Kelvin Makamba, baada ya mshambuliaji wao Issa Simbaliawa kufanyiwa madhambi na mlinzi wa Tanesco.
Bao la pili lilipachikwa katika dakika ya 32 na Ramadhani Shegodo aliyepata krosi safi kutoka kwa Idd Likasi.
Timu za soka zimegawanywa katika makundi mawili, ambapo kila kundi litatoa timu mbili zilizoshika nafasi za juu, na zitacheza hatua ya nusu fainali na fainali.
Mbali na soka michuano hiyo inashirikisha michezo ya netiboli, kuvuta kamba, karata, draft na bao kwa wanawake na wanaume.

Kesho timu ya kamba wanawake ya Tanesco itaumana na NAO, huku katika soka RAS Iringa watacheza na Hifadhi ya Ngorongoro katika uwanja wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa, na timu ya Uchukuzi itakutana na Ngorongoro katika mchezo wa netiboli utakaofanyika Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) na timu ya kamba ya wanawake ya Uchukuzi itavutana na MUHAS.

No comments:

Post a Comment