Saturday, October 14, 2023
LIGI YA NBC CHAMPIONSHIP LEAGUE YALAMBA UDHAMINI MNONO
Na Rahel Pallangyo
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeingia mkataba wa miaka mitatu na TV 3 wenye thamani ya Sh. Milioni 613, kwa ajili ya haki za kurusha NBC Championship League.
Udhamini wa TV 3 umekuja siku chache baada ya kupata mdhamini mkuu ambaye ni benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni miaka 11 imepita bila mdhamini.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, Rais wa TFF Wallace Karia alisema wameingia mkataba wa kuonesha mubashara NBC Championship League kwa sababu inawasaidia kila kitu kuwa hadharani na kupunguza malalamiko yasiyo na msingi.
Alisema watafanikiwa kuona timu ambazo zinatumia mambo maovu kwa ajili ya kujinufaisha lakini pia kubaini malalamiko ya timu zinazolalamika kufanyiwa maovu na kuwataka viongozi wa klabu kutumia fursa hiyo kujitafutia wadhamini binafsi.
“Nina imani wadhamini wetu hao hawatajutia kabisa kufanya kazi na TFF na nitahakikisha wanapata kipaumbele inapotokea fursa nyingine,"
Karia alisema ligi hiyo ni kati ya ligi ngumu nchini na kuishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani.
"Kuonesha kwa Ligi Kuu kupitia Azam TV imekuwa hamasa kubwa kwa kuifanya iwe bora, matarajio yangu kwa mkataba huu tulioingia na TV 3 kwa ajili ya kuonesha mechi ya Championship itafanya pia kuwa bora zaidi na kuleta wadhamini wengine,” alisema Karia.
“Tutakuwa wakali kwa klabu ambazo hazijajianda kucheza daraja la juu, niwaombe wapambane kutafuta wadhamini ili kujimudu katika ligi wanayoshiriki, TFF sio kazi yao kuwatafutia klabu wadhamini,” alisema.
Naye Msimamizi wa vipindi wa TV3, Emmanuel Sikawa alisema mkataba huo ni hatua kubwa kwao kwa sababu wanatarajia kuonesha mechi 170 kati ya 240 ambazo zitachezwa katika ligi hiyo.
Alisema ligi hiyo itaonueshea katika chanel mbili ambazo ya 197 kwa upande wa Dish na 131 kwa Antena, ambazo zinaruka nchi saba.
“Tunatarajia ligi itaoneshwa katika mataifa hayo saba ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda , Afrika Kusini, Uganda, Burundi na Msumbiji ikiwa ni lengo la kutangaza ligi hii na wachezaji kuonesha vipaji vyao na kuonekana kujiuza kwa kutazamwa,” alisema Sikawa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment