LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Manchester United, Alex Ferguson amewaambia majirani zake Manchester City: Kama mnataka maneno ya kuchezeana akili nipo tayari.
SIR. ALEX FERGUSON
Kocha huyo ameongeza kuwa kitendo cha kumrudisha Carlos Tevez katika kikosi kwenye hatua za lala salama kinaonyesha ni kwa kiasi gani majirani zake wamechanganyikiwa.
Ferguson aliongeza kuwa yeye ndiye bingwa wa kucheza na akili za wapinzani na kama wanataka mchezo huo, yupo tayari.
Mwanzoni mwa wiki hii, kiungo za zamani wa Manchester City, Patrick Vieira, alisema kuwa kitendo cha Manchester United kumrudisha Paul Scholes licha ya kwamba alikuwa amestaafu kinaonyesha ni kwa kiasi gani wamechanganyikiwa, lakini Fergie amekanusha.
"Ukiangalia kwa makini utaona majirani zetu ndio wamechanganyikiwa, inawezekana vipi mchezaji akatae kuingia uwanjani, halafu kocha atamke kwamba hatacheza tena, kibaya zaidi mchezaji huyo anaondoka bila kuaga, baada ya muda anarudi na kusamehewa, hiyo inamaanisha nini?" alihoji.
Ferguson alijigamba kuwa anatarajia kuwa na kikosi imara zaidi baada ya Chris Smalling, Phil Jones, Fabio, Tom Cleverley na Paul Pogba kuimarika.
"Kwa sasa tunasubiri kuona Nani na Michael Owen wakikaa sawa tayari kwa mapambano ya mwisho."
No comments:
Post a Comment