BUKOBA SPORTS

Saturday, April 21, 2012

EL CLASCO HISPANIA: NI KAMA FAINALI YA LA LIGA

Ile mechi murua kabisa, 'El Classico' hatimaye imewadia. Na safari hii, itakapopigwa leo Jumamosi, inatarajiwa kuwa ni moja ya mechi muhimu sana  kuchezwa mwaka huu kwa timu zote mbili; Barcelona na Real Madrid.
Barcelona watajitupa uwanjani huku wakijua, kuwa ni LAZIMA washinde ili wawe na matumaini ya kiuhalisia kuwa wanaweza kutwaa taji la ubingwa wa Ligi ya Hispania kwa mwaka huu.
Hadi sasa, Real Madrid  wako mbele ya Barcelona kwa pointi nne huku mechi ya leo Jumamosi itaamanisha zitakuwa  zimebaki mechi nne kabla ya ligi ya Hispania kumalizika.
Juzi hapa Real Madrid wamechapwa na  Bayern Munich kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Vivyo hivyo kwa Barcelona, nao pia wamechapwa na Chelsea.  Timu zote mbili; Barcelona na Real Madrid, zitakuwa zikiingia uwanjani  zikiwa zimejeruhiwa.
Kwa vile Real Madrid imeitangulia Barcelona kwa pointi nne, inavyoonekana, hawatataka  Barcelona wapate ushindi na kufanya tofauti yao iwe ya pointi moja tu huku wakiwa wamebakisha mechi nne za kucheza kwa kila mmoja wao.
Mechi ya mwisho ya El Classico iliyowakutanisha Barcelona na Real Madrid ni ya kwenye Copa Del Rey mwaka huu.  Matokeo katika mechi hizi mbili za El Classico  ni Barcelona kumfunga Real Madrid  2-1 kwenye uwanja wa nyumbani wa Real Madrid, na waliposhuka kucheza pale Camp Nou,  matokeo yakawa sare ya 2-2.
 Mechi hizi mbili zilizowakutanisha vigogo hawa wa soka ulimwenguni zilikuwa ngumu sana na za kuvutia.
Mechi ya leo Jumamosi itachezwa kwenye uwanja wa  Camp Nou. Ni uwanja wa nyumbani wa Barcelona. Ifahamike, kuwa Barcelona,
katika msimu huu,  hawajapoteza hata mechi moja kwenye uwanja wao wa nyumbani. Barca wamekuwa mahodari sana kila wanapocheza kwenye uwanja wao huku wakishangiliwa na mashabiki wao.

Kuna mechi ambazo Barcelona imepoteza ilipocheza ugenini, lakini, mara zote wamehakikisha wanautumia vema uwanja wao wa nyumbani. Katika msimu mzima wametoa sare moja tu nyumbani.

Wakati huo huo, Real Madrid wanajua, kuwa  kama watashinda hiyo kesho, basi, itakuwa ni kama wameshatawazwa ubingwa wa Ligi ya Uhispania. Kitakachobaki ni mteremko tu. Basi, mechi ya kesho ni kama ' fainali' ya Ligi ya Hispania.
Kwa Real Madrid mechi ya leo Jumamosi haihusiani na ushindi tu wa uwanjani. Bali, ushindi kwa Madrid utakuwa na maana kubwa kisaikolojia kwa timu hiyo.
Hii ni kwa sababu, Real Madrid ikiwa na kocha Mourinho imeifunga mara moja tu Barcelona. Ni kwenye michuano ya Copa Del Rey mwaka jana. Hivyo, ushindi kwa Real Madrid kesho utaisaidia timu hiyo katika kujiamini zaidi kila wanapokutana na Barcelona badala ya wachezaji kutanguliza  hofu zaidi ya kupoteza mchezo. Kwamba hata wao wanaweza kuwafunga Barcelona kama watakutana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Ushindi kwa Madrid leo pia utawapa nguvu za ' kisaikolojia' kwa kujiamini kuwa wanaweza kuwaangusha Bayern Munich kwenye mechi ya marudiano Jumanne ijayo itakayopigwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Real Madrid. Na umuhimu huo anaujua vema kocha wa Real Madrid, Jose  Mourinho.

Na moja ya silaha kubwa ya Real Madrid dhidi ya Barcelona leo itakuwa kwenye benchi la ufundi la Real Madrid.
Kocha Mourinho anaijua vizuri sana Barcelona. Klabu zote alizozifundisha Mourinho zimekutana na Barcelona mara kadhaa chini ya kocha huyo.

Sifa moja kubwa ya kocha Mourinho ni  uwezo wake wa kuchagua kutoka kwenye hazina ya wachezaji wake, wachezaji sahihi kucheza kwenye mechi sahihi. Si kila mchezaji anaweza kucheza mechi yeyote ile, hata kama ni mchezaji nyota. Kuna mechi zinazohitaji aina fulani ya wachezaji.
Na kama nilivyoweka wazi hapo juu, kwa kocha Mourinho, hakuna klabu anayoijua zaidi Ulaya kama Barcelona. 
 Akiwa na Real Madrid, Mourinho ameifunga Barcelona mara moja, lakini, ametoka sare nne na Barcelona, na kwa vile Mourinho ni ' mtaalamu' wa kutoka sare, basi ni matokeo ya sare ndiyo anayoyahitaji leo.
 Hii ni kwa sababu, sare itawaongezea Madrid pointi moja na kuwafanya waendelee kuongoza ligi kwa ponti nne mbele ya Barcelona huku kukiwa kumesalia na mechi nne kumaliza ligi.

Kati ya wachezaji muhimu kwa Real Madrid  ni pamoja na Christian Ronaldo aliyepachika hadi sasa,  mabao  41 ya Ligi kwenye ligi ya  Hispania. Xabi Alonso pia ni karata muhimu kwa Real Madrid. Huyu ndiye anayetarajiwa kupewa jukumu la kuvuruga mfumo mzima wa pasi za Barcelona uwanjani.


Kwa  Barcelona, silaha yao kubwa  si nyingine bali inaitwa ' Lionel Messi'. Kwa pamoja, Messi na Ronaldo wana idadi sawa ya mabao ya kufunga kwenye Ligi ya Hispania.

Lakini, kwa sasa Messi yuko vizuri zaidi kimchezo zaidi ya Ronaldo. Kati ya sifa zake nyingi, Messi ana uwezo wa kukimbia kwa kasi huku akiumiliki mpira. Bila  shaka, Messi atawapa wakati mgumu sana mabeki wa Madrid.
Kwa kawaida, Messi anaweza kuanzisha mwenyewe mashambulizi akitokea nyuma. Ana uwezo mkubwa pia wa kuwatengenezea wachezaji wenzake vyumba muhimu uwanjani vitakavyowapa nafasi za kufunga mabao. Ana uwezo wa kurudi nyuma na kuhami mashashambulizi ya adui.

Wachezaji wengine muhimu sana kwa Barcelona hapo  ni Xavi na Iniesta. Hawa ndio ' injini' ya Barcelona. Ni mahodari wa kutoa pasi za uhakika na kukimbia wakiwa na mpira.
Utabiri wangu:
Kwa kuziangalia timu hizi mbili na rekodi zao za muda mrefu  na za hivi karibuni, nawaona  Barcelona wakitoka washindi kwenye mechi .
Na hasa kwa vile, Barcelona watajitupa uwanjani hiyo kesho huku wakijua wanakwenda kucheza mechi muhimu sana ya ligi.

Na Barca wataibuka washindi wakisaidiwa na rekodi yao ya kustaajabisha ya kutopoteza hata mechi moja msimu huu kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Nadhani pia, kuwa  Real Madrid hawana kile kinachohitajika kuwafunga Barcelona,
na hawakuwa nacho walipocheza na Bayern Munich na hata wakapoteza mechi yao.
 Real Madrid bado ni mkusanyiko wa nyota wa dunia ambao wakati mwingine hawatoi kile cha mwisho katika kuipigania na hata kuifia timu uwanjani. 
Ikumbukwe pia, kama kocha, Jose Mourinho, akiwa na vilabu tofauti, amefungwa mara saba na Barcelona.  Jumamosi inaweza kuwa ni kwa mara yake ya  nane.

No comments:

Post a Comment