BUKOBA SPORTS

Friday, April 20, 2012

FIFA YAMUONYA DENIS OLIECH KWA MGOMO WAKE WA KUTOICHEZEA TIMU YA TAIFA

          DENIS OLIECH


FIFA imeonya kuwa inaweza kumchukulia hatua za kinidhamu Nahodha wa Timu ya Taifa ya Kenya, Dennis Oliech, kwa uamuzi wake wa kujitoa kuchezea Nchi hiyo.
Oliech, anaecheza Klabu ya Ufaransa Auxerre, amejitoa kwenye Timu ya Kenya ambayo inatakiwa kujitayarisha kucheza na Togo hapo Juni 16 kwenye mechi ya mchujo kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
Sababu za Oliech kujiondoa Timu ya Kenya ni kufuatia mzozo ambapo yeye anadai apewe mgao unaotokana na udhamini wa Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki, East African Breweries Limited, lakini Shirikisho la Soka Kenya, Football Kenya Federation, FKF, limedai Mchezaji huyo hana haki hiyo kwa vile hamna kipengele hicho kwenye Mkataba na Mdhamini.
Mwenyekiti wa FKF, Sam Nyamweya, amedai: ‘Mkataba unawaruhusu Wadhamini kutumia picha za Timu ya Taifa katika matangazo. Lakini sasa tunaongea nao upya ili nao Wachezaji wanufaike.’
Akitoa ufafanuzi, Mkurugenzi wa Sheria wa FIFA, Marco Villiger, amesema Mchezaji anaesusa kuchezea Timu ya Taifa anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Hadi sasa upo mgogoro mwingine unaomhusu Staa mwingine wa Kenya, MacDonald Mariga, anaechezea Klabu ya Serie A huko Italia, Parma, ambae anaidai FKF zaidi ya Shilingi Milioni 1 za Kenya kwa kujilipia mwenyewe Nauli wakati akienda kujiunga na Timu ya Taifa ya Kenya.

No comments:

Post a Comment