BUKOBA SPORTS

Friday, April 20, 2012

JUMAMOSI EL CLASCO HAPATOSHI, NI MESSI V RONALDO


Licha ya kuwa ndio Mechi ambayo inaweza kuamua hatma ya Ubingwa wa La Liga Msimu huu, ‘El Clasico’ ya Jumamosi hii, kama inavyobatizwa Mechi kati ya Mahasimu Barcelona na Real Madrid, ni Mechi ambayo pia inaleta ushindani mkubwa wa kufunga mabao kwa Nyota wa Timu hizo, Lionel Messi wa Barca na Cristiano Ronaldo wa Real.
Vinara wa Ligi ni Real ambao wako Pointi 4 mbele ya Mabingwa watetezi Barca huku Mechi zikiwa zimebaki 5 kabla hawajakutana Jumamosi Uwanjani Nou Camp na Mastaa Messi na Ronaldo ndio wamefungana kwa ufungaji bora wote wakiwa na goli 41 kila mmoja ikiwa ndio rekodi ya ufungaji bao nyingi katika La Liga kwa Msimu mmoja.
Msimu uliopita Ronaldo ndie alievunja rekodi kwa kupachika bao 40 na Msimu huu amefunga bao 53 katika Mechi zote za Mashindano yote wakati Messi, ambae ndie amemrithi Ronaldo kama Mchezaji Bora Duniani na kuitwaa Tuzo hiyo mara 3 mfululizo hadi sasa, amepiga jumla ya bao 63 katika Mashindano yote na kwenye UEFA CHAMPIONZ LIGI ndie anaongoza kwa kufunga bao 14 Msimu huu.
Ikiwa Messi atafunga zaidi ya goli 67 basi ataivunja rekodi ya kufunga bao nyingi katika Msimu mmoja Barani Ulaya iliyowekwa na Straika wa Ujerumani aliekuwa akichezea Bayern Munich, Gerd Muller, aliyoiweka Msimu wa Mwaka 1972/3.
Ingawa Klabu hizi zote Wiki hii zimefungwa ugenini kwenye Mechi za kwanza za Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI, kwa Real kuchapwa 2-1 na Bayern Munich na Barca kutunguliwa 1-0 na Chelsea, lakini upo uwezekano kwa wao kukutana Fainali kwa vile Mechi za marudio zipo kwao Spain.
Wakiwa ndio Mabingwa wa Spain kwa Miaka mitatu mfululizo, Barcelona Msimu huu tayari wameshawashinda Real Madrid kwenye Super Cup na Copa del Rey na pia kuwachapa bao 3-1 Uwanjani Santiago Bernabeu kwenye Mechi ya La Liga Mwezi Desemba.

JOSE_MOURINHOLicha ya kuwa ni Mechi kubwa yenye jina mahsusi, El Clasico, na kuwa na Masupastaa wa Dunia,PEP_GUARDIOLA Messi na Ronaldo, Mechi hii pia ina mvuto wa kiaina yake kwa kuwa na Mameneja wenye hulka tofauti kwa Barca kuwa na Mtu makini na muungwana Pep Guardiola na Real kuwa na Meneja machachari, aliejibatiza jina la ‘Mtu Spesheli’, Jose Mourinho.
Ushindani wote huu na pia kuwa na Mameneja hao huwa kunaleta mfarakano ambao haukosi lawama za Refa kupendelea na Kadi Nyekundu kutembea na hata kutiana vidole machoni kitu kilichoshuhudiwa pale Jose Mourinho alivyomtovuga Kocha Msaidizi wa Barca, Tito  Vilanova, mwanzoni mwa Msimu huu.
Mbali ya Klabu hizi kuwa na uhasama pia upo uhasama wa kihistoria unaohusisha maeneo Klabu hizi zilipo.

Head to head Lionel Messi versus Cristiano Ronaldo

Barca wao wanatoka Jimbo la Catalonia ambalo linataka uhuru na huichukulia kama Serikali iliyo na Makao Makuu Mjini Madrid, wanakotoka Real Madrid, kama ni wadhalimu kwao.
Msuguano huu, na vita hii, pia imedakwa na Magazeti ambapo Magazeti maarufu ya Jijini Madrid, Marca na As, yapo upande wa Real Madrid, na yale ya Mjini Barcelona, Sport na El Mundo Deportivo, ni mashabiki wa Barca.
Na hivi karibuni ujio wa Jose Mourinho umeongeza chumvi zaidi hasa kwa vile ‘Mtu Spesheli’ aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa Barcelona katika Miaka ya 1990 wakati Kocha wa sasa wa Barcelona Pep Guardiola akiwa Mchezaji wa Klabu hiyo.
Tangu Mourinho atue Real kama Kocha akitokea Inter Milan hapo Mwaka 2010 ameishinda Barcelona mara moja tu katika Mechi 10 na siku zote amekuwa akidai Barca wanabebwa na Marefa.
Mourinho aliwahi kutamka: ‘Guardiola ni Mtu mwerevu na anajua wazi kwa nini ameweza kushinda Mechi nyingi. Anajua fika hilo limetokeaje!’
Timu yeyote itakayoshinda hiyo Jumamosi itakuwa imefikisha ushindi wa Mechi 87 katika jumla ya Mechi 219 kati yao tangu waanze kukutana Mwaka 1902 kwenye Copa del Rey na huku sare zikiwa 46.
Real Madrid wao wanahitaji kufunga bao moja tu ili waivunje ile rekodi ya bao 107 kwa Msimu mmoja iliyowekwa na wao wenyewe wakiwa chini ya Kocha kutoka Wales, John Toshack, Msimu wa Mwaka 1989/90.



Kwenye La Liga, Real Madrid na Barcelona, zimeziacha mbali sana Timu nyingine na Timu iliyo nafasi ya 3 Valencia ipo Pointi 29 nyuma ya Barcelona ambao wapo nafasi ya pili.

No comments:

Post a Comment