Jose Mourinho, meneja wa Real Madrid ya Uhispania, amesema angelipenda Chelsea ya Uingereza ipate ushindi itakapocheza na Bayern Munich katika mechi ya fainali ya soka ya klabu bingwa mjini Munich.
Chelsea walifuzu kuingia fainali baada ya kuishinda Barcelona, pia ya Uhispania, na kwa muda mrefu wakicheza wakiwa 10.
"Bila shaka ningelipenda Chelsea wawe washindi. Walikuwa ni mashujaa kuishinda Barcelona wakiwa na wanaume kumi uwanjani," alisema meneja huyo wa zamani wa The Blues.
"Mimi ninajivunia wachezaji wangu, lakini katika mechi kubwa kama hiyo, tulihitaji nguvu zaidi na tulipaswa kuwa wachangamfu."
Kutokana na wachezaji wa timu zote kufanya makosa ambayo ililazimika mwamuzi kuwaadhibu katika mechi za nusu fainali, Bayern Munich na Chelsea zote zitawakosa wachezaji mahiri.
Bayern itazikosa huduma za David Alaba, Holger Badstuber na Luiz Gustavo.
Chelsea nayo itacheza pasipo Ramires, John Terry, Branislav Ivanovic na Raul Meireles kuingia uwanjani.
Lakini licha ya Real kuanza kwa kasi, na hasa baada ya kuwashinda wapinzani wao wakuu Barca katika ligi kuu ya nyumbani ya La Liga mwishoni mwa wiki, walishindwa kupata bao la ushindi dhidi ya Bayer, ambyo iliweza kuwatumia wachezaji waliokuwa wamepata nafasi ya kupumzika, baada ya ubingwa wa Bundesliga kuchukuliwa na Borussia Dortmund.
"Lazima uweze kuwa katika hali ya wastani, iwapo utashinda au utashindwa," Mourinho alisema.
"Vijana walicheza vizuri, na kiakili wakiwa imara, na wakitambua walikuwa wanacheza na timu kali, na timu ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa likizoni.
"Tulishindwa, tunahuzunika, na wao wamefurahi, lakini hiyo ndio hali ya kandanda."
No comments:
Post a Comment