Kwa miaka mingi Kenya ilikuwa inashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika katika idadi ya medali ilizokuwa inapata kwenye mashindano ya Olimpiki.
Hata hivyo wanamishezo wa nchi hiyo wamefanya vibaya kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni mjini London Uingereza.
Kenya mwaka huu imeporomoka hadi nafasi ya tatu kwenye orodha ya nchi za Afrika zilizopata medali katika Michezo ya Olimpiki.
Ukitoa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1996 iliyofanyika Atlanta Marekani, Kenya imekuwa ikipata medali nyingi zaidi kwenye michezo hiyo tangu mwaka 1968.
Matumaini ya Kenya kuendelea kuongoza kwa kuwa na medali nyingi za Olimpiki barani Afrika yalipotea baada ya wanariadha wake watatu kushindwa kupata medali za dhahabu katika mbio za masafa marefu yaani marathoni wanaume, zilizofanyika juzi Jumapili.
Badala yake, mkimbiaji kutoka Uganda, Stephen Kiprotich aliwafadhaisha wanariadha mashuhuri wa Kenya kama vile Wilson Kipsang na Emmanuel Mutai walioambulia medali za fedha na shaba, nyuma ya Kiprotich aliyepata medali ya dhahabu.
Nayo nchi jirani ya Tanzania iliendeleza historia yake ya kuvurunda katika Michezo ya Olimpiki kwa wanamichezo wake kurejea nyumbani mikono mitupu wakishindwa kupata angalau medali moja ya shaba.
Mashindano yajayo ya Olimpiki yatafanyika nchini Brazil mwaka 2016.
kutoka http://kiswahili.irib.ir/ michezo
No comments:
Post a Comment