BUKOBA SPORTS

Monday, October 8, 2012

LAMPARD, GIBBS HATARINI KUIKOSA SAN MARINO.


Kiungo nyota wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Chelsea, FRANK LAMPARD kuna hatihati ya kutocheza mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya San Morino Ijumaa ijayo baada ya kuumia katika mchezo ambao timu yake iliibuka kidedea kwa kuifunga mabao 4-1 Norwich.Beki wa klabu ya Arsenal, KIERAN GIBBS naye pia anaweza kuwa nje ya uwanja katika mchezo huo baada ya kutolea nje mapema katika kipindi cha pili wakati timu yake ilipoibika na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham United Jumamosi. Katika mchezo wa Chelsea ambao ulipigwa katika Uwanja wa Stamford Bridge, LAMPARD alifunga bao la pili na kufikia rekodi yaBOBBY TAMBLING aliyewahi kufunga mabao 129 lakini alionekana wazi kusumbuliwa na maumivu wakati alipotolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Ramires katika dakika ya 23 ya mchezo huo. Akihojiwa kuhusiana na hali ya mchezaji huyo meneja wa klabu hiyo ROBERTO DI MATTEO kwa muda huo asingeweza kufahamu lakini baada ya madaktari wa timu hiyo kumfanyia uchunguzi ndio watatoa majibu ya nini kinamsumbua kiungo huyo. Kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo ROY HODGSON ambaye alikuwepo uwanjani hapo kuwafuatilia LAMPARD na ASHLEY COLE atakuwa na amepatwa na mfadhaiko baada ya kumuona nahodha wake huyo ambaye amechukua nafasi ya STEVEN GERARD anayetumikia adhabu kuukosa mchezo dhidi ya San marino.

COLE KUCHUKULIWA HATUA CHELSEA.
Meneja wa klabu ya Chelsea, ROBERTO DI MATTEO amefafanua kuwa mchezaji ASHLEY COLE anaweza kupewa adhabu na klabu hiyo baada ya kutuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akiiponda Chama cha Soka cha Uingereza-FA. COLE mwenye umri wa miaka 31 alituma ujumbe mara baada ya Baraza Huru la FA kutoa utetezi wake ambao ulimkuta mchezaji mwenzake JOHN TERRY na hatia ya kumfanyia vitendo vya kibaguzi beki wa Queens Park Rangers ANTON FERDINAND. Akihojiwa kuhusiana na tukio hilo DI MATTEO amesema kuwa klabu hiyo ina sera zake kuhusiana na mitandao ya kijamii hivyo ni wazi kutakuwa na hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa kwa COLE na yeye hataweza kuingilia. Beki huyo wa kushoto alituma ujumbe wa kuitukana FA kwa uamuzi waliotoa lakini baadae aliufuta ujumbe huo ingawa hata hivyo Chelsea imepanga kumchukulia hatua na pia anaweza kupambana na adhabu nyingine kutoka FA. DI MATTEO hajawazuia wachezaji wake kutumia mitandao ya kijamii lakini amewaonya kuwa inaweza kuwaletea matatizo kama wasipotumia uhuru huo vizuri.



AL AHLY YALAZIMISHWA SARE NA SUNSHINE LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

Mabingwa mara sita wa Afrika, Al Ahly ya Misri wamelazimishwa sare ya mabao 3-3 na Sunshine Stars ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa katika Uwanja wa Dipo Dina mjini Ijebu-Ode, Nigeria. Katika mchezo huo Sunshine ilimkosa nahodha wake GODFREY OBOABONA ambaye alikuwa akitumikia adhabu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Esperance wakati MOHAMED ABOUTRIKA naye alikosa mchezo huo baada ya kufungiwa miezi miwili na klabu yake ya Al Ahly. Katika mchezo huo mabao ya Al Ahly yalifungwa na MOHAMED NAGY aliyefunga mabao mawili na MAHDY EL SAYED huku mabao ya Sunshine yalifungwa na TAMEN MEDRANO, DELE OLORUNDARE kwa njia ya penati na PRECIOUS OSASCO. Nusu fainali nyingine inatarajiwa kuchezwa leo jijini Lubumbashi ambapo mabingwa mara mbili TP Mazembe itaikaribisha Esperance ya Misri ambapo washambuliaji nyota wa kimataifa kutoka Tanzania MBWANA SAMATTA na THOMAS ULIMWENGU wanatarajiwa kuingoza Mazembe kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
_____________________________________________________________

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.


MISRI NAYO YAIKACHA SERENGETI BOYS
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imefuzu kucheza raundi ya tatu nay a mwisho kwenye michuano ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Vijana baada ya Misri kujitoa. Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya pili dhidi ya Misri; mchezo wa kwanza ukichezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam na ule wa marudiano wiki mbili baadaye jijini Cairo. Katika raundi ya kwanza Serengeti Boys inayofundishwa na Jakob Michelsen kutoka Denmark ilikuwa icheze na Kenya mwezi uliopita, lakini nchi hiyo ilijitoa katika michuano hiyo ambayo fainali zake zitachezwa Machi mwakani nchini Morocco. Serengeti Boys sasa itacheza raundi ya tatu kwa kumkabili mshindi wa mechi kati ya Zimbabwe na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itachezwa Novemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika ugenini wiki mbili baadaye. Zimbabwe na Congo Brazzaville zitapambana zitapambana kati ya Oktoba 12-14 mwaka huu, Zimbabwe ikiwa mwenyeji wa mechi ya kwanza wakati ya marudiano itafanyika kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.

LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA SITA
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwan wa Tanzania Bara inaingia raundi ya sita wikiendi hii kwa mechi saba. Kesho (Oktoba 6 mwaka huu) African Lyon itakuwa mwenyeji wa Azam katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Nayo Ruvu Shooting itaikaribisha Coastal Union ya Tanga katika mechi itakayochezeshwa na Oden Mbaga wa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani. Mbaga atasaidiwa na Samuel Mpenzu, Ferdinand Chacha na Andrew Shamba. Jumapili (Oktoba 7 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Simba na Oljoro JKT itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kagera Sugar na Yanga (Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba), Mgambo Shooting na Polisi Morogoro (Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga), Toto Africans na JKT Ruvu (Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza) na Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya).

No comments:

Post a Comment