BUKOBA SPORTS

Friday, January 25, 2013

ARSENE WENGER: UHAMISHO JANUARI UFUTWE AU USIZIDI WACHEZAJI WAWILI

BOSI wa Arsenal Arsene Wenger ametaka Dirisha la Uhamisho la Mwezi Januari lifutwe kabisa au libakishwe kwa kuruhusu Uhamisho wa Wachezaji wawili tu kwa kila Klabu kwa vile mfumo wa sasa hautendei haki Klabu nyingine.
Amesema: “Si haki kwani baadhi ya Timu zishacheza, kwa mfano na Newcastle, na nyingine bado kukutana nayo halafu wanacheza nao huku wakiwa na Wachezaji 6 au 8 wapya!”
Aliongeza: “Nadhani Uhamisho huu ufutwe au Klabu zisinunue Wachezaji zaidi ya wawili!”
Mtindo wa Madirisha ya Uhamisho ulianzishwa kwenye Msimu wa 2002/03.
Katika Kipindi hiki cha Uhamisho Arsenal haijasaini Mchezaji yeyote mbali ya kuvumishwa kutaka kuwachukua David Villa wa Barcelona na Mohamed Diame wa West Ham Wachezaji ambao Wenger amekanusha kujaribu kuwachukua.
Akitolea mfano wa Newcastle ambao kwenye Dirisha hili la Uhamisho wa Mwezi Januari tayari limewanasa Massadio Haidara, Yoan Gouffran, Mapou Yanga-Mbiwa na Mathieu Debuchy huku Moussa Sissoko kutoka Klabu ya Toulouse akiwa njiani kujiunga, Wenger alisema: “Timu ambazo hazijacheza na Newcastle hazitakutana na Timu ile ile!”
Hadi sasa Wenger hajafuta kuwa hawezi kusaini Mchezaji mpya Mwezi huu lakini amekiri kuwa akitokea Mchezaji mzuri ambaye anapatikana watamchukua tu.
Wenger amesisitiza: “Kitu ambacho kinanitatiza ni kuwapata tena majeruhi wetu na kuwafanya Wachezaji wote wacheze kwa uwezo wao wote. Hatutegemei miujiza toka nje, tunategemea mafanikio toka ndani ya Klabu. Ikitokea Mtu anaweza kuimarisha Kikosi chetu tutamchukua tu lakini kwa sasa tuna Wachezaji wawili kwa kila pozisheni na hiyo inatosha! Lakini, tukipata Mchezaji wa kiwango cha juu Duniani hatukatai kumchukua!”

No comments:

Post a Comment