Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen, ametaja Kikosi cha Wachezaji 21
kitakachoingia Kambini Jumapili Februari 3 kwa ajili ya Mechi ya
Kirafiki dhidi ya Cameroun itakayochezwa Jumatano Februari 6, Siku ya
Kalenda ya FIFA, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
PATA TAARIFA KAMILI:
Release No. 018
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Januari 31, 2013
KIM ATEUA 21 STARS WA KUIVAA CAMEROON
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen
ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili
(Februari 3 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon
(Indomitable Lions).
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar
es Salaam leo (Januari 31 mwaka huu), Kim amesema mechi dhidi ya
Cameroon itakuwa kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi
kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco
itakayofanyika Machi mwaka huu.
“Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi
kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya
maandalizi kabla ya mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu
wachezaji wameonyesha wako tayari.
“Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na
Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo
mechi dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika
huko,” amesema Kim ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini
kuzifuatilia timu za Morocco na Ivory Coast zilizo kundi moja na
Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi
lake nyuma ya Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo
ni Gambia.
Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake
ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula
(Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey
Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari
Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon
Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum
Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi
Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana
Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment