Shirikisho la mchezo wa soka
duniani FIFA, limethibitisha kuwa limepokea malalamishi kutoka kwa
shirikisho la mchezo wa soka nchini Malawi FAM, kuhusiana na matamshi
yaliyotolewa na kocha wa Nigeria, Stephen Keshi.
Hata hivyo shirikisho hilo la FIFA limesema kuwa
kwa sasa haliwezi kusema lolote kuhusu suala hilo, hadi uchunguzi
utakapo kamilika.
FAM limedai kuwa Keshi alitoa matamshi ya ubaguzi dhidi ya kocha wake Tom Sainfiet raia wa Ubelgiji.
Katibu mkuu wa FAM, Suzgo Nyirenda ameiambia
BBC, kuwa matamshi hayo ya ubaguzi hayafai kuwepo katika michezo katika
dunia ya sasa.
''Tunahisi na shambulio dhidi ya kocha wetu na
tutamtetea kwa hali na mali, bila kuzingatia uraia wake na rangi ya
ngozi yake'' Alisema Nyirenda.
''Tumetuma ushahidi wa yale Keshi aliyoyasema na
tunatarajia kuwa FIFA itachukua hatua kali dhidi ya kocha huyo wa
Nigeria Stephen Keshi'' aliongeza Nyirenda.
Kesi hiyo inahusiana na matamshi ambayo Keshi
aliyatoa kufuatua wito wa Malawi wa kuhamisha mechi yao ya kufuzu kwa
kombe la dunia mwaka wa 2014, kutoka mji wa Calabar kutokana na sababu
za kiusalama.
Katika mahojiano na runinga moja ya Uingereza, Keshi alisema ''Nafikiria kuwa kocha huyo wa Malawi ni wazimu''.
''Ikiwa anataka kuongea na FIFA, basi ni lazima
arejea kwao nchini Ubelgiji. Yeye sio mtu wa Afrika, ni mzungu mweupe,
ni lazima arudi kwao Ubelgiji'' Alisema Keshi katika mahojiano hayo.
Maafisa wakuu wa shirikisho la mchezo wa soka
nchini Nigeria pamoja na kocha huyo hawajasema lolote kuhusiana na madai
hayo ya kocha wa Malawi Saintfiet na FAM.
Mechi hiyo kati ya Malawi na Nigeria mjini
Calabar itaamua nani atafuzu kwa raundi ya mwisho ya mechi ya kufuzu kwa
fainali hiyo barani Afrika.
Mabingwa hao wa Afrika wanahitaji kutoka sare ya aina yoyote ili kufuzu ili hali Malawi inahitaji ushindi ili isonge mbele.
No comments:
Post a Comment