Kawaida Fainali za Kombe la Dunia huchezwa Mwezi Juni na kumalizika mapema Julai lakini kipindi hicho huko Qatar ni Joto kali linalofikia Digrii 50 Centigrade.
Hii leo, Makamu wa Rais wa ECA, Umberto Gandini, amesema kuwa wao wako tayari Fainali hizo zibadilike kwa mara hiyo moja tu lakini nyingine zote ziwe wakati ule ule Mwezi Juni.
ECA wana Mkutano wao kuanzia Jumanne na uamuzi huu unatarajiwa kupitishwa rasmi.
Hivi karibuni kumekuwa na Mjadala mkali kuhusu kuchezwa Fainali hizo Majira ya Joto huko Qatar na Wasimamizi wa Ligi Kuu England walipinga kubadilishwa huko lakini Siku chache zilizopita Mkuu wa FA, Chama cha Soka England, Greg Dyke, alisema wao wanaunga mkono kuzibadilisha Fainali hizo ili zichezwe Majira ya Baridi.
Mwezi ujao FIFA inacho Kikao chao ambacho kinatarajiwa kupendekeza Fainali hizo za Mwaka 2022 zibadilishwe na kuchezwa Majira ya Baridi huku Rais wa FIFA, Sepp Blatter, akisema ni 'Ubaguzi' kushikilia Fainali hizo zichezwe Mwezi Juni tu.
Blatter amethibitisha kuwa kwenye Kikao cha Kamati ya Utendaji ya FIFA kitakachofanyika Oktoba 3 na 4 huko Zurich, Uswisi yeye atapendekeza Fainali za Mwaka 2022 zibadilishwe na kuchezwa Mwezi Novemba na Desemba.
Blatter ametamka: "Ikiwa tutakuwa na msimamo mkali na kung'ang'ania hali hii hii, basi Fainali za Kombe la Dunia haziwezi kuchezwa kwenye Nchi za Kusini ya Ikweta au zile za Ikweta. Kwa hili tunazibagua Nchi ambazo zina Majira tofauti na Ulaya. Sasa umefika wakati wa Ulaya kuelewa hawaitawali tena Dunia na wale Wakoloni wa zamani hawawezi tena kulazimisha Nchi za mbali."
No comments:
Post a Comment