RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameunda kamati mbili maalumu kwa ajili ya kutathmini muundo wa ligi na kupendekeza namna ya kuboresha.
Pia kamati hizo zitatathmini muundo wa Bodi ya Ligi na kupendekeza namna ya kuuboresha ikiwemo kuunda kampuni ambayo itakuwa na kazi ya kusimamia/ kuendesha ligi.
Akizungumza na wandishi wa habari, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Boniface Wambura ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu, alisema kuwa Kamati ya Kutathmini Muundo wa Ligi inaongozwa na Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla wakati Katibu ni Ofisa Mashindano wa TFF, Idd Mshangama. Wajumbe ni Rahim Kangezi, Amri Said, Sunday Manara, Salim Bawazir na Lucas Kisasa.
David Nchimbi kutoka Delloitte ndiye anayeongoza Kamati ya Muundo wa Bodi ya Ligi wakati wajumbe ni Edwin Kidifu (Mwanasheria wa SUMATRA), Jones Paul (Mkurugenzi wa Sunderland/Symbion Academy), Evans Aveva, John Jambele, Masoud Sanani na Pelegrinius Rutahyuga.
Pia Rais Malinzi amemteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa Mshauri wa Rais kwenye masuala ya Ufundi wakati Mshauri wa Rais kwenye mambo ya Utawala atateuliwa baadaye.
Wakati huo huo jopo la wataalamu 20 walioteuliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi linakutana kupanga mkakati wa kuonesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2015 nchini Morocco.
Kikao hicho maalumu (retreat) kitafanyika mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6-8 mwaka huu chini ya Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu.
Wengine ni makocha Dk. Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah Kibaden, Pelegrinius Rutahyuga, Kidao Wilfred, Salum Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Boniface Mkwasa, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay na Dan Korosso na wajumbewengine toka Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).
No comments:
Post a Comment