BUKOBA SPORTS

Wednesday, May 28, 2014

RAIS MALINZI ATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA KOCHA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso Mwale.
Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha Mwale, na kuongeza kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano wa kuigwa kwa makocha wazalendo waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.

Rais Malinzi amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mwale, na kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwao.

Mwale (51) alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha katika barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini kujiunga na timu yake kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment