BUKOBA SPORTS

Saturday, October 17, 2015

HAPATOSHI LEO TAIFA: MABINGWA YANGA KUIVAA AZAM FC LIGI KUU VODACOM! REFA NI ABDALLAH KAMBUZI!

BAADA ya kuwa Vakesheni Wiki 2 kupisha Mechi za Kimataifa, VPL, Ligi Kuu Vodacom Leo inarejea kilingeni na Bigi Mechi ipo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam wakati Mabingwa Yanga watakapocheza na Azam FC iliyomaliza Nafasi ya Pili Msimu uliopita.
Baada ya Mechi 5 za VPL, Yanga na Azam FC ndio Timu pekee ambazo hazijafungwa na zote zina Pointi 15 kila mmoja lakini Yanga wako kileleni kwa ubora wa Magoli.
Msimu huu, hii itakuwa ni mara ya pili kwa Yanga na Azam FC kukutana baada ya kucheza Mechi ya kufungua pazia la Msimu huu mpya kugombea Ngao ya Jamii ambayo Yanga waliibeba baada ya kushinda kwa Penati 8-7 baada ya Sare ya 0-0 katika Dakika 90.
Kabla ya hapo, Mechi ya mwisho kucheza kwa Timu hizi ilikuwa kwenye Robo Fainali ya Kagame Cup ambayo Azam FC waliibuka kidedea kwa kuitoa Yanga kwa Penati 5-3.
Yanga chini ya Kocha Mholanzi Hans van Pluijm, akisaidiwa na Kocha mpya Juma Mwambusi, Leo itakosa huduma ya Kiungo wao kutoka Rwanda Haruna Niyonzima ambae yuko kwao akila raha za fungate baada ya kuoa.

Nao Azam FC, chini ya Kocha Mwingereza Stewart Hall, wana Timu imara na Kikosi kamili bila upungufu wa Majeruhi.
Timu hizi zina Difensi imara kwenye Ligi ambazo haziruhusu Mabao kirahisi kwani baada ya Mechi 5 Yanga imefungwa Bao 1 tu wakati Azam FC imefungwa Bao 2 tu.
Kila Timu ina Fowadi hatari huku Yanga wakiongozwa na Mzimbabwe Doland Ngoma na Mrundi Amis Tambwe ambao hadi sasa kila mmoja ana Bao 4 wakisaidiwa na Malimi Busungu na Simon Msuva ambae ndie alizoa Buti ya Dhahabu Msimu uliopita kwa kuibuka Mfungaji Bora wa VPL.
Lakini pia Fowadi ya Azam FC ni moto ikiwa na Mtu 3 hatari ambao ni John Bocco, Kipre Tchetche na chipukizi Faridi Mussa.

Nalo Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza Viingilio vya Mechi hii ya Leo ya Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam ambapo kiingilio cha chini ni Shilingi Elfu 5 kwa viti vyenye rangi ya Bluu, Kijani na Machungwa.
Tiketi za mchezo huo zitauzwa Leo Jumamosi katika eneo la Uwanaja wa Taifa, Dar es salaam, ambapo kingilio cha juu kitakua ni Shilingi Elfu 30 kwa VIP A, na Shilingi Elfu 20 kwa VIP B & C.

Mwamuzi wa mchezo huo atakuwa Abdallah Kambuzi kutoka Shinyanga, akisaidiwa na Makame Mdogo (Shinyanga), Robert Luhemeja (Mara), Mwamuzi wa Akiba ni Frank Komba (Dar es Salaam) huku Kamisaa akiwa Joseph Mapunda kutoka Ruvuma.

Mbali ya Mechi hii ya Yanga na Azam FC, Vigogo wengine wa Tanzania, Simba, Leo wako Ugenini huko Mjini Mbeya Uwanja wa Sokine kuwavaa Watoto wa Nyumbani Mbeya City mbao Leo ni Mechi yao ya kwanza tangu Kocha wao Juma Mwambusi ahamie Yanga.

No comments:

Post a Comment