BUKOBA SPORTS

Tuesday, May 29, 2018

SIMBA YAKABIDHIWA MILIONI 100 NA SPORTPESA

MABINGWA wa Tanzania klabu ya Simba imekabidhiwa hundi ya Sh. Milioni 100 na kampuni ya SportPesa Tanzania baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
SportPesa Tanzania, ambao pia ni wadhamini wa mahasimu wa Simba, Yanga na Singida United imetekeleza kipengele cha mkataba wao kinachosema timu itakayotwaa ubingwa wa Ligi Kuu itapewa kiasi hicho cha fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo, Oysterbay, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa kampuni hiyo, Abbas Tarimba aliwapongeza viongozi na wachezaji wa Simba kwa kutwaa ubingwa kwani wameitendea haki nembo ya SportPesa
“Awali ya yote niwapongeza viongozi na wachezaji wa Simba kwani mmewapa heshima kubwa wana msimbazi kote nchini na kubwa zaidi ni heshima mliyotupa sisi kama wadhamini wenu wakuu, Simba imeitendea haki nembo yetu ya SportPesa na kampuni inaamini kuwa wadhamini wakuu imekuwa ni moja ya chachu iliyosababisha Simba kuchukua ubingwa huu,” alisema Tarimba
“Tunachokifanya leo ni kutimiza moja ya ahadi tuliyotoa wakati tunasaini mkataba Mei mwaka jana kuwa tutatoa bonasi ya Sh Milioni 100 endapo mojawapo ya timu tunazozidhamini itachukua ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo bila shaka timu ni Simba”, aliongeza Tarimba
Pia Tarimba amewataka viongozi kupeleke kikosi kamili kwenye michuano ya SportsPesa Super Cup inayotarajia kuanza Juni 3-10 nchini Kenya ili iweza kuwa bingwa na kurudi na kitita cha dola za Kimarekani 30,000 pamoja na kupata nafasi ya kwenda nchini Uingereza kucheza na Everton FC ya Ligi Kuu ya England Uwanja wa Goodison Park.
Naye Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Iddi Kajuna aliishukuru SportPesa kwa kuleta mabadiliko kwenye soka nchini ambapo wao wameyaona kwa upande wao.
“Niwashukuru SportPesa kwa kuleta mabadiliko ya soka nchini ambayo sisi Simba tumeyaona na tutaendelea kutoa ushrikiano katika miaka mingine minne iliyosalia kwenye mkataba wetu”, alisema Kajuna
Simba ni miongoni mwa timu nne kutoka Tanzania zitakazoshiriki michuano ya SportPesa Super Cup itakayofanyika nchini Kenya kuanzia Juni 3-10 ambayo yatashirikisha timu nane
Timu nyingine ni Yanga, Singida United na JKU ya Zanzibar, kutoka Kenya ni timu za Gor Mahia, AFC Leopards, Kakamega Home Boys na Kariabangi Sharks za Kenya. Gor Mahia ndiye bingwa mtetezi wa michuano hiyo baada ya kuwafunga watani wao wao jadi, AFC Leopard katika fainali mwaka jana zilizofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment