BUKOBA SPORTS

Saturday, May 12, 2012

TWIGA STARS, ZIMBABWE KUUMANA LEO UWANJA TAIFA

 
Wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Zimbabwe, wakiwa katika mazoezi ya pamoja kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya mchezo wao wa kesho kati yao na Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania Twiga Stars, mchezo ubaotarajia kupigwa kesho katika Uwanja wa taifa jijini.
Wachezaji wa Zimbabwe wakiwa mazoezinini jana.
 Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) na Zimbabwe zinapambana leo (Mei 12) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars ambayo ilikuwa katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza imerejea leo (Mei 11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam tayari kuikabili Zimbabwe. Ikiwa Mwanza jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi Rock City Queens, lakini mechi hiyo ilivunjika dakika ya 58 kutokana na mvua kubwa. Hadi mechi inavunjika, Twiga Stars ilikuwa ikiongoza kwa mabao 5-0.

Kwa mujibu wa kocha wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa, mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi ya mashindano ya Afrika (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya kurudiana Dar es Salaam wiki mbili baadaye.


Naye Kocha wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza amesema amefurahi kupata mechi hiyo kwa vile anaamini Twiga Stars ni kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi yao ya AWC dhidi ya Nigeria.

Twiga Stars na Zimbabwe zilishakutana mara mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.
Mechi ya pili ilikuwa michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba kuanzia saa 10.30 jioni ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.

No comments:

Post a Comment