Fulbeki wa Manchester United Rafael Da Silva amesaini Mkataba mpya utakaomweka Klabuni hapo hadi Mwaka 2016.Habari hizi zimetobolewa na Wakala wa Rafael, Cassiano Pereira, ambae amesema Mbrazil huyo ana furaha kubwa kuendelea kubaki Old Trafford na kucheza Mechi kubwa Ulaya akiwa na Klabu kubwa Duniani.
Rafael, mwenye Miaka 21, alijiunga Man United akitokea Fluminense Mwaka 2008 akiwa na Pacha mwenzake Fabio, na hivi sasa yupo kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa ya Brazil alikoitwa baada ya kuumia Dani Alves na kucheza Mechi mbili za kirafiki.
Akimzungumzia Fabio, Wakala Cassiano Pereira amesema Mchezaji huyo atachezea QPR iliyo Ligi Kuu England kwa mkopo Msimu ujao ili apate uzoefu zaidi kwa vile amekuwa hana namba kwenye Kikosi cha kwanza cha Man United.
Pereira amesema: “Fabio ni Kijana mwenye kipaji na tumekubaliana na Sir Alex Ferguson aende kwingine kwa mkopo ili apate uzoefu. Alipata ofa za huko Germany na Portugal lakini ameamua abaki England ili aendeleze staili ile ile ya uchezaji ili akirudi Man United iwe rahisi kwake.”
No comments:
Post a Comment