BUKOBA SPORTS

Tuesday, July 24, 2012

JUMA KASEJA: TUPENI SAPOTI MSITUZOMEE KAGAME CUP!


NAHODHA wa Simba, Juma Kaseja, amewataka wapenzi na wanachama wa Simba kutofanya vitendo vya kuwakatisha tamaa wachezaji katika wakati huu ambapo timu inashiriki katika Kombe la Kagame.
Akizungumza na tovuti ya Simba, Kaseja alisema katika wakati huu ambapo kuna shinikizo kubwa kwa wachezaji, ni muhimu kwa wapenzi na wanachama kuwa kitu kimoja.
“Watu wanatakiwa kuelewa kwamba timu yetu hii ndiyo kwanza imeanza mazoezi na wachezaji ndiyo wanafahamiana. Hakuwezi kuwa na mabadiliko ya ghafla.
“Hata msimu uliopita, timu ilikuwa inapanda kiwango taratibu. Nashangaa kuna wapenzi wa Simba ambao wanaizomea timu yao ikifanya vibaya. Wao wanatakiwa kutusapoti na si kutuvunja nguvu,” alisema.
Alisema kwenye mechi yoyote ile, wachezaji wa Simba wanakuwa wamejiandaa kuzomewa na washabiki wa Yanga lakini hawatarajii kukatishwa tamaa na washabiki wao.
“Inawezekana mchezaji wa Simba akakosea lakini shabiki wa timu yake anatakiwa kumpa moyo na si kumponda. Wachezaji wengine wanahitaji kupewa moyo ili wafanye vizuri, wakikatishwa tamaa mapema, ndiyo hawatacheza tena,” alisema.
Kaseja ambaye amekuwa mlinda mlango namba moja wa Simba kwa takribani miaka nane sasa, aliunga mkono maelezo ya Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic, kuwa Simba itatisha msimu ujao wa ligi.
Alisema kwa namna anavyoona, Simba itakuwa nzuri zaidi msimu huu kuliko msimu uliopita lakini cha msingi ni kwa wapenzi na wanachama kuwa na subira.

MRWANDA ATAWAZIBA MIDOMO WOTE
DANI MRWANDA
MCHEZAJI mwandamizi wa Simba amewaonya washabiki wanaoponda kiwango cha mshambuliaji Dani Mrwanda kuwa watakuja kufunga midomo yao hivi karibuni.
Akizungumza na tovuti ya Simba, nahodha wa Simba, Juma Kaseja, alisema kiwango cha Mrwanda hakijashuka isipokuwa anahitaji muda midogo kurejea kwenye kiwango chake.
“Mimi nashangaa watu wanaoponda kiwango cha Dani. Mimi nakuhakikishia kabisa kwamba Mrwanda atacheza na tena atacheza vizuri kwenye timu hii. Wale wote wanaombeza kwa sasa, watajutia maneno yao,” alisema Kaseja.
Alisema mchezaji mzuri kama Dani hawezi kuonekana mbovu eti kwa sababu alicheza vibaya kwenye mechi moja tu wakati uzuri wake unajulikana kwa miaka mingi.
Kaseja alisema kwa jinsi anavyofahamu yeye, Mrwanda ameathiriwa na kutocheza kwa muda mrefu tangu mkataba wake wa Vietnam ulipokwisha miezi michache iliyopita.
“Mara baada ya mkataba wake kwisha, alirejea nchini na hakufanya mazoezi sana. Sasa amepata timu na ndiyo ameanza mazoezi rasmi. Akiwa fiti tu, mtamwona Mrwanda mliyemzoea,” alisema.

Source:http://www.simba.co.tz

No comments:

Post a Comment