CAF CHAMPIONS LEAGUE: MAZEMBE WAIZIDI MAARIFA AL AHLY NA KUIPIGA 2-0, SAMATTA ANG'ARA.
MABINGWA mara nne wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, TP Mazembe wamefanikiwa kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga mabao 2-0 Al Ahly ya Misri katika mchezo uliochezwa jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC. Matokeo hayo ya jana yanamaanisha timu ya Berekum Chelsea ya Ghana imeenguliwa katika michuano hiyo ya ngazi ya juu kwa vilabu barani Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zamalek. Mabao ya Mazembe yalifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta na Deo Kanda katika kipindi cha pili na kuendeleza uteja kwa Al Ahly ambao wameshindwa kutamba kwao katika mara zote walizokutana. Timu zote mbili zimefikisha alama 10 hivyo kuongoza katika kundi B huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na Berekum Chelsea wenye alama tano huku wakiwa wamebakisha mchezo mmoja wa mwisho. Katika mchezo wa mwisho Al Ahly italazimika kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya mahasimu wao Zamalek na kuomba TP Mazembe wapoteze mchezo wao dhidi ya Berekum Chelsea ili waweze kusonga mbele kama vinara wa kundi lao ili kuepuka kukutana na Esperance ambao wanaongoza kundi A katika nusu fainali ya michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment