REFA CLATTENBURG NA KESI YA CHELSEA, KIBAO CHAWAGEUKIA BLUES, MAREFA KUIGOMEA!!?
>>FA Kufungua Mashitaka dhidi ya Chelsea!
Wakati Chelsea wamewakilisha rasmi malalamiko yao kwa FA, Chama cha Soka England, na Kikundi cha Wanasheria Weusi kikipeleka malalamiko Polisi kuhusu tuhuma za kauli ya Kibaguzi ya Refa Mark Clattenburg dhidi ya Wachezaji wa Chelsea, John Mikel Obi na Juan Mata, wakati wa Mechi ya Ligi Kuu England iliyochezwa Stamford Bridge Jumapili iliyopita na wao kuchapwa 3-2 na Man United, huku Mameneja magwiji Arsene Wenger na Sir Alex Ferguson wakishangazwa mno na tuhuma hizo, kumeibuka taarifa kuwa Marefa wanafikiria kuigomea Chelsea ili kumuunga mkono mwenzao.
Habari za ndani toka FA zinadai kuwa Chelsea imevunja Kanuni kadhaa ambazo kwanza ziliwataka wasisogelee Chumba cha Marefa hadi baada ya Dakika 30 baada ya Mechi lakini wao walimvamia Refa Mark Clattenburg Dakika 15 tu baada ya Mechi na tena bila ruksa ya kumuona.
Wakati hayo yanaibuka, Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, amedai Chelsea hawakupaswa kulalamika bali wangemaliza tatizo lolote kati yao chemba bila kuhusisha mtu.
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, akiongea hapo jana, alisema: “Hamna Refa atakaejishusha chini kufanya kitendo kile. Nina hakika na hilo. Katika Miaka 15 iliyopita hakuna hata Mchezaji mmoja aliekuja kwangu na kudai Refa alimwapiza au kumkashifu. Ingawa gemu ya leo na ile ya Miaka 25 iliyopita imebadilika, mwenyewe nimecheza Soka na najua nini kinaendelea katika Mechi kati ya Wachezaji na Refa na vingi vimebadilika sasa.”
Nae Meneja wa Fulham, Martin Jol, amesema: “Kama Refa huyo alitamka hayo basi ni ujinga lakini siamini alisema hivyo!”
Akichangia, Meneja wa QPR, Mark Hughes, ametaka sakata hilo limalizwe haraka ili lisileta madhara makubwa.
Wakati huo huo, kumeibuka taarifa kuwa Marefa wanafikiria kuigomea Chelsea ili kuonyesha kumuunga mkono mwenzao Mark Clattenburg.
Refa wa zamani Clive Wilkes ameeleza: “Nina mawasiliano mazuri na Marefa wengi na wote wanamsapoti Clattenburg. Wapo wanaoongelea kuigomea Chelsea. Marefa wanahisi hawasaidiwa na hili limewachanganya sana. Wanahisi wakilalamika watafutwa na Mgomo ndio njia yao ya mwisho!”
No comments:
Post a Comment