TAARIFA KWA UMMA
UCHAGUZI WA VIONGOZI WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA NA TANZANIA PREMIER LEAGUE BOARD (TPL)
KUSITISHA ZOEZI LA KAMPENI
12/02/2013
1. Kamati ya Uchaguzi, kwa mamlaka
iliyonayo kupitia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 3(1), 6(1) (g) na
(l), 10(5), 11(6) inayosomeka pamoja na Ibara ya 14(1) na (2) na pia
Ibara ya 26(5) na (6), imesitisha zoezi la kampeni za uchaguzi wa TFF na
TPL Board lililokuwa lianze kesho tarehe 13/02/2013 hadi hapo
itakapowatangazia, ili kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakidhi
kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.
2. Tarehe za Uchaguzi Mkuu wa TFF na TPL Board zinabaki kama zilivyopangwa.
3. Taarifa hii inazingatia pia Ibara ya
2(4) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF inayoagiza uongozi uliopo madarakani
kuendelea na kutekeleza majukumu ya Shirikisho hadi hapo mchakato wa
uchaguzi utakapokamilika.
Deogratias Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI TFF
Release No. 026b
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 12, 2013
UCHAGUZI FRAT UPO PALEPALE FEB 14
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha
Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) unafanyika Februari 14 mwaka
huu mjini Morogoro kama ulivyopangwa, tofauti na taarifa wanazopewa
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya
Uchaguzi ya FRAT, Damas Ndumbaro, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa FRAT
wanatakiwa kufika Morogoro keshokutwa (Februari 12 mwaka huu) . Pia
wapiga kura na wagombea wanatakiwa kulipia ada za uanachama kwa mwaka
2013 kabla ya uchaguzi.
Wagombea ni Army Sentimea na Said
Nassoro (uenyekiti) wakati wanaoomba nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Juma
Chaponda, Juma Mpuya na Tifika Kambimtoni.
Abdallah Mitole, Charles Ndagala na
Hamis Kisiwa wanawania ukatibu mkuu, nafasi ya Mhazini inagombewa na
Jovin Ndimbo. Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ni Kamwaga Tambwe wakati nafasi ya uwakilishi wanawake
yupo Isabela Kapera.
Wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Emmanuel Chaula na Samson Mkotya.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Release No. 026
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 12, 2013
WASHABIKI WAZIUNGE MKONO AZAM, SIMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linawaka washabiki wa mpira wa miguu kujitokeza kwa wingi wikiendi
hii kuzishangilia timu za Azam na Simba zitakazocheza mechi za
mashindano ya Afrika jijini Dar es Salaam.
Nguvu ya washabiki ni muhimu katika
kuziweza timu hizo kufanya vizuri katika mechi hizo za nyumbani dhidi ya
Al Nasir Juba ya Sudan Kusini na Club Libolo ya Angola.
Azam itacheza Jumamosi (Februari 16
mwaka huu) dhidi ya Al Nasir katika mechi ya Kombe la Shirikisho wakati
Simba itaikabili Club Libolo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
itakayofanyika Jumapili. Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
LYON, YANGA KUUMANA UWANJA WA TAIFA
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inamaliza raundi ya 16 kesho (Februari 13 mwaka
huu) kwa mechi kati ya wenyeji African Lyon dhidi ya Yanga
itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakayochezshwa na mwamuzi
Martin Saanya kutoka Morogoro inakutanisha timu zenye mazingira tofauti.
Wakati Yanga wakiwa ndiyo vinara wa ligi hiyo kwa pointi 33, African
Lyon ambayo sasa inanolewa na Salum Bausi inakamata mkia ikiwa na pointi
tisa tu.
Nayo Toto Africans itaikaribisha Polisi
ya Morogoro kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mechi
itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma. Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000 utakuwa
mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Oljoro JKT.
Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky
Maxime ambaye sasa ni kocha wa Mtibwa Sugar ataiongoza timu yake hiyo
katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu ulioko
Turiani, Morogoro. Ni kwenye uwanja huo huo ambapo Mtibwa Sugar katika
mechi yao iliyopita walichapwa mabao 4-1 na Azam.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment