Monday, August 26, 2013

KAMATI KUU YA CCM YAMZUIA KAGASHEKI KUSHIRIKI SHUGHULI ZA KISIASA BUKOBA MJINI.

DODOMA. 
SUALA la kutimuliwa kwa madiwani wanane wa CCM katika Manispaa ya Bukoba limeingia sura mpya baada ya Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kushiriki katika siasa mkoani humo hadi mwaka 2015.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubain
ika mgogoro wa viongozi hao, unakiumiza chama katika jimbo hilo.

Taarifa zilidai chanzo cha ugomvi kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani, ni kwa kila mmoja kutaka kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Bukoba mjini katika uchaguzi ujao. Na kwa uamuzi huo, Kagasheki na Dk Amani hawatashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema viongozi hao watakutana na Kamati Kuu leo na baada ya hapo utatangazwa uamuzi uliofikiwa.

Mbali na meya na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, wengine walioitwa katika kikao hicho cha leo ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Costansia Buhinye, katibu wake, Averin Mushi pamoja na mwenyekiti wa chama Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na katibu wake, Janath Kayanda.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu ambayo ilimaliza kikao chake saa 8:30 usiku wa kuamkia jana italazimika kukaa tena leo kuwaelezea uamuzi uliofikia.

Kumekuwapo na mgogoro mkubwa katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, ukimuhusisha Kagasheki na baadhi ya madiwani kwa upande mmoja; na Dk Amani na kundi jingine la madiwani kwa upande mwingine.

Wakati wa mgogoro huo madiwani wamekuwa wakituhumiana ufisadi, na CCM imekwishawatuma viongozi wake wa juu kuingilia kati mgogoro huo akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana.

Kufikishwa kwenye Kamati Kuu kwa suala hilo kumekuja baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kuamua kuwatimua uanachama madiwani hao, hatua ambayo ilikuwa inahatarisha nafasi zao na hivyo kukiingiza chama hicho kwenye uchaguzi mdogo.

Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi hao kuwajibishwa kwa kukiuka kanuni, kwa kuwa upo uamuzi wa chama unaokataza viongozi waliochaguliwa katika vyombo vya dola kuwajibishwa kwa staili hiyo.

Madiwani waliovuliwa uanachama na kata zao katika mabano ni pamoja na Richard Gaspar (Miembeni ), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai).

Wengine ni Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment