BUKOBA SPORTS

Sunday, September 29, 2013

KLABU YA BARCELONA YATHIBITISHA KUUMIA KWA LIONEL MESSI, ATAKUWA NJE KWA WIKI 3!

Mchezaji nyota wa Barcelona Lionel Messi atakuwa nje ya Uwanja kwa wiki mbili hadi tatu akijiuguza matatizo ya Musuli za Paja lakini anatarajiwa kupona na kuwepo kwenye El Clasico.
Jumamosi, Messi, Miaka 26, ilibidi atolewe nje ya Uwanja katika Dakika ya 29 Barcelona walipocheza Ugenini Mechi ya La Liga na Almeria yeye akiwa tayari ameshafunga Bao 1 na hatimae Barca kushinda 2-0 kwa Bao la Pili la Adriano Correia.
Leo, Klabu ya Barcelona imetangaza kuwa Messi ataikosa Mechi ya Jumanne ya UEFA CHAMPIONZ LIGI Ugenini na Celtic na pia Mechi ya Jumamosi ijayo Oktoba 5 ya La Liga dhidi ya Valladolid itakayochezwa Uwanja wa Nou Camp.

Baada ya Mechi hiyo ya Oktoba 5, hamna Mechi za La Liga hadi Oktoba 18 kwa vile kati yake kutakuwa na Mechi za Kimataifa kwa mujibu wa Kalenda ya FIFA.
Hivyo, Barca wanategemea Messi atarudi tena Uwanjani kwenye Mechi yao inayofuata ambayo ni ya La Liga hapo Oktoba 18 Ugenini na Osasuna na Wiki moja baadae ndio El Clasico Uwanjani Nou Camp wakati Real Madrid watakapotua hapo.
Kwa muda sasa Messi amekuwa akikabiliwa na tatizo la maumivu ya aina hiyo lakini hilo halijamzuia kuisaidia Barcelona kushinda Mechi zao zote 7 za La Liga Msimu huu huku yeye akifunga Bao 8 hadi sasa.

No comments:

Post a Comment