BUKOBA SPORTS

Saturday, November 30, 2013

KOCHA MPYA WA AZAM ATAMBULISHWA, KUANZA KAZI JUMATATU


Kocha mpya wa Azam akikabidhiwa jezi na Mzee Said leo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo

Kocha Joseph Omog akiwa ameshika jezi aliyokabidhiwa

Mzee Said akiongea na waandishi wa habari leo


Kocha na mzee Said wakiwasili kwenye chumba cha mkutano kuzungumza na waandishi wa habari

KOCHA Joseph Omog amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha klabu ya Azam kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa mwakani.
Omog raia wa Cameroon, amewasili nchini leo na moja kwa moja akasaini mkataba wa miaka miwili wa kuwafundisha wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), akichukua mikoba iliyoachwa na Stewart Hall.

Hall alitangaza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo baada ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.


“Tumepitia historia na uzoefu wake tukaone tumpe jukumu la kuifundisha timu yetu kwa kipindi cha miaka miwili,” alisema Mwenyekiti wa Klabu ya Azam, Said Mohamedi

“Historia yake inaonesha kuwa ana uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya kimataifa, kwani aliwahi kuiwezesha Leopards ya Congo Brazaville kutwa kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), mashindano ambayo timu yetu itashiriki.

Mohamedi alikataa kuweka wazi kiwango cha fedha atakacholipwa kocha huyo kwa hoja ya kwamba hiyo ni siri baina ya klabu hiyo na kocha huyo.

Akizungumza kwenye utambulisho huo, Omog alisema kuwa ana furaha kupewa jukumu la kuifundisha Azam na kusema kuwa ni timu anayoifahamu kwani aliiona wakati ikishiriki mashindano ya Kombe la CAF mwaka jana.

“Jukumu langu ni kuona kuwa timu hii inafanya vizuri kwenye ligi na pia kwenye mashindano ya Kombe la CAF, lakini hilo litawezekana kutokana na ushirikiano kutoka kwa wachezaji na viongozi wa timu hii,” alisema Omog aliyekuwa akizungumza kwa lugha ya kifaransa na mwanae Henry Omog ambaye ndiye Meneja wake kutafsiri kwa lugha la Kiingereza.

No comments:

Post a Comment