
KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam ipo katika mkakati wa kujenga kiwanda cha kisasa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zinazohusiana na kazi za wasanii.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Alex Msama alisema Dar es Salaam juzi kuwa kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa mkombozi kwa wasanii wa aina mbalimbali ambao wamekuwa wakipata tabu kupata malighafi zinazohusiana na kazi zao. “Badala ya kuhangaika nje ya nchi kupata CD au DVD au mambo mengine yanayohusiana na kazi za wasanii, sisi tutakuwa tunatengeneza hapahapa Tanzania kwa ubora mzuri zaidi.
“Tumejipanga katika hili na tayari kuna kampuni ya China tumefikia hatua nzuri kwa ajili ya jambo hili na mapema mwezi ujao nitaenda huko kwa hatua za mwisho za mazungumzo ya ujenzi wa kiwanda hicho.
“Kitakuwa kiwanda cha kisasa ambacho naamini wasanii Watanzania watakifurahia na kitawapunguzia gharama katika kuandaa kazi zao na hilo tunalifanya kwa nia njema kabisa kuhakikisha tunawasaidia wasanii,” alisema Msama ambaye pia Kampuni yake pia inaandaa Tamasha la Pasaka.
Alisema awali lengo la kuanzisha kampuni yake lilitokana na kugundua kwamba muziki wa Injili bado uko nyuma na haujapiga hatua nchini kulinganisha na nchi nyingine kama Afrika Kusini. "Niliamua kuanzisha Msama Promotions baada ya kuona muziki wa Injili umesahaulika na unashuka thamani yake, hivyo tukaona ni busara kuuinua ili tuwe kama wenzetu Afrika Kusini ambao wana waimbaji wa nyimbo za Injili wanaotamba kama Rebecca Malope, Steve Kekane, Vuyo Mokoena na wengine wengi," alisema.
“Hili la kuuweka katika jamii muziki wa Injili tumefanikiwa sana, hivi sasa nguvu zetu zipo katika kuanzisha kiwanda cha kuzalisha kazi mbalimbali zinazohusiana na kazi za wasanii. Zitakuwa bidhaa nyingi sana sitaweza kuzitaja zote,” alisema Msama.
No comments:
Post a Comment