Murage Kabange, kocha msaidizi wa Kagera Sugar amesema kuwa katika mechi tano walizobakiza wamejiandaa kupata ushindi ili kutetea nafasi yao ya nne au kupata ya tatu.

“Mwaka jana tuliishia nafasi ya nne. Msimu huu tumekuwa na majeruhi wengi. Kikubwa kwasasa tunajipanga kuibuka na ushindi katika michezo yote iliyosalia”.
“Malengo yetu ilikuwa ni kutwaa ubingwa au kushika nafasi ya pili. Kushuka nafasi ya nne hatukutarajia. Lakini kutokana na matatizo ya kikosi chetu, sasa tunaiwinda nafasi ya tatu au kusalia nafasi ya nne kama mwaka jana”. Alisema Kabange.
Kocha huyo alisema maandalizi yao kuelekea mchezo wa jumapili dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Kaitaba yanakwenda barabara,hivyo wana matumaini ya kufanya vizuri.
“Tunanoa makali ya safu ya ushambuliaji ili kuipa makali. Pia tunarekebisha kasoro zilizopo safu ya kiungo na ulinzi.
Tunatarajia kufanya vizuri dhidi ya Ruvu Shooting”. Alisema Kabange.
Akizungumzia mechi tano zilizosalia, Kabange alisema wanahitaji kujiandaa kwa umakini mkubwa kwasababu kuna ushindani wa hali ya juu.

“Hukuna mechi nyepesi hata kidogo. Tunacheza na Ruvu Shooting jumapili. Baada ya hapo tutawasubiri Simba nyumbani. Mechi hizi kwanza ukiziangalia zitakuwa ngumu, lakini tunafanya maandalizi mazuri”. Aliongeza Kabange.
Baada ya mechi hiyo, watasafiri mpaka Tanga kuwavaa Mgambo JKT uwanja wa Mkwakwani aprili 13 mwaka huu.
Kibarua chao cha mwisho ni aprili 19 dhidi ya Coastal Union uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.
Mpaka sasa, Kagera Sugar wameshuka dimbani mara 21 na kujikusanyia pointi 32 katika nafasi ya 5.
Mbele yao wapo wekundu wa Msimbazi Simba ambao wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 36 katika nafasi ya nne.
No comments:
Post a Comment